RAS BALANDYA AAHIDI USHIRIKIANO ZAIDI NA JIJI LA WURZBURG- UJERUMANI
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndg. Balandya Elikana amewapokea waheshimiwa Madiwani na watendaji kutoka Halmashauri ya Jiji la Wurzburg- Ujerumani na kuwahakikishia ushirikiano zaidi na Jiji la Mwanza kwa faida ya wananchi wa pande zote mbili.
Akizungumza na wageni hao Ofisini kwake mapema leo asubuhi Novemba 08, 2024 mtendaji huyo wa Mkoa amebainisha Jiji la Wurz burg limekuwa na miradi mingi ya kijamii Jijini Mwanza yenye lengo la kuwaletea maendeleo wananchi hivyo hakuna budi kuudumisha ushirikiano huo.
"Tunatambua baadhi ya miradi inayofadhiliwa na Jiji la Wurzburg ikiwemo mradi maji safi huko kisiwa cha Ijinga wilayani Magu, vifaa tiba na mafunzo kwa wataalamu wa afya kwenye hospitali ya Nyamagana, uwekaji wa umeme wa mwanga wa jua kwenye jengo la Halmashauri ya Jiji la Mwanza na ujenzi wa madarasa na maktaba shule ya msingi Butimba hii ni miradi yenye kuwaletea tija ya maendeleo wananchi",Balandya.
Aidha amesema Serikali ya Mkoa wa Mwanza inazidi kupiga hatua ya kuwaondelea umasikini wananchi wake kwa kuwawezesha miradi mbalimbali ukiwemo ufugaji wa samaki kwa njia ya vizimba kwa kupitia mikopo isiyo na riba.
Kiongozi wa msafara huo uliowajumuisha Madiwani na Meya,Bi Babra Lehrieder amemshukuru mwenyeji wake kwa mapokezi mazuri na kubainisha lengo la ujio wao ni kujionea miradi hiyo na kuhakikisha inazidi kuwa na ustawi mzuri kwa wananchi hali itakayoleta maana zaidi ya ushirikiano baina ya majiji hayo.
Katika ziara hiyo Madiwani hao wataitembelea pia nyumba ya kihistoria ya Gunzet house iliyopo katikati ya Jiji la Mwanza ambayo ilijengwa na wakoloni wa kijerumani kwa lengo la kujihami na adui ambayo awali waliifanyia ukarabati wa zaidi ya shs milioni 200 ili iwe na mvuto zaidi wa kitalii kama eneo la makumbusho.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.