Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amewataka wahitimu kuwa mabalozi wazuri wa chuo chao kwa kufuata waliyofundishwa darasani na kuzingatia weledi, ujuzi na nidhamu haswa katika jamii zinazowazunguka.

Amesema hayo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza katika mahafali ya 51 ya chuo cha usimamizi wa fedha (IFM) katika kampasi za Mwanza, Simiyu na Geita yaliyofanyika leo Disemba 6, 2025 katika ukumbi wa Rockcity mall manispaa ya Ilemela.

Ameendelea kwa kuwataka wahitimu hao kutumia mradi wa elimu ya juu wa mageuzi ya kiuchumi (HEET) wenye lengo la kukuza elimu ya juu kama chachu ya kuleta uchumi mpya wa Tanzania.

Kadhalika amewaasa wahadhiri wa IFM kuendelea kuwafundisha vyema wanafunzi wanaoendelea na kwa juhudi kubwa ili kuendelea kuboresha mitaala na kuendana na mahitaji mbalimbali.

Aidha ametoa wito kwa uongozi wa chuo cha IFM kuendelea kutoa elimu yenye ubora na kuendelea kuzalisha wataalamu huku akisisitiza kuongeza kozi za kufundisha katika kampasi za kanda ya ziwa kwani zitaenda kuongeza wataalamu na kupunguza changamoto mbali mbali katika jamii.

Awali akisoma risala Mkuu wa chuo cha IFM Prof. Josephat Lotto ameishukuru serikali kwa misaada ya fedha na miongozo ambayo imesaidia katika kuhakikisha wanaziendeleza kampasi za Mwanza, Geita na Simiyu lakini pia kwa kukipatia chuo nafasi za kuajiri watumishi mbalimbali.

Naye mwenyekiti wa baraza la uongozi wa chuo Prof. Emmanuel Mjema ameiomba serikali iweze kuwasaidia kuongeza nguvu katika ukuzaji wa rasilimali watu huku akisema kuwa ujenzi wa chuo na mabweni katika kata ya Kisesa unaendelea kwa kiwango cha kuridhisha, na amewasihi wahitimu waweze kujiendeleza kielimu ili kuendelea kukuza utambuzi na uelewa.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.