RAS MWANZA AZITAKA HALMASHAURI KUTENGA FEDHA KUSIMAMIA MPANGO WA M-MAMA
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Daniel Machunda amezitaka Halmashauri zote za Mkoa huo kutenga bajeti za kutekeleza mpango wa M-Mama unaotekeleza rufaa kwa ajili ya matibabu kwa wajawazito, waliojifungua na watoto ili kukomesha vifo vitonanavyo na uzazi.
Bwana Machunda ametoa wito huo mapema leo Agosti 17, 2024 wakati akifungua kikao kazi cha kujadili uendelevu wa mfumo wa usafirishaji wa wajawazito, waliojifungua na watoto kwenda kupata huduma za afya M- Mama katika hoteli ya Adden Palace Ilemela.
Aidha, ameagiza vituo vya afya kuweka mikakati thabiti ya upokeaji wa rufaa na waratibu wa zoezi hilo kusimamia kwa weledi na wakati ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya wakati wote na kuhakikisha Taifa linakua na uzazi salama wakati wote.
"Vifo vitokanavyo na uzazi vinaumiza sana, ni lazima tuhakikishe kujifungua kunakua ni neema na sio janga kwa jamii kwani ni jambo la neema tulilopewa na Mwenyezi Mungu", amesisitiza ndugu Machunda ambaye ni Katibu Tawala Msaidi sehemu ya Utawala na Usimamizi wa rasilimali watu.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Jesca Lebba amesema mfumo wa usafirishaji wa dharula kwa wajawazito, waliojifungua pamoja na watoto una miezi 18 tangu kutambulishwa Mwanza na rufaa zilianza kwa kupiga namba 115 na kwamba Serikali imeshirikiana na wadau wakati wote kufanikisha rufaa.
Aidha, amesema pamoja na majukumu mengine waratibu wamekagua na kuweka vifaa kwenye uratibu wa kituo cha kupokelea wagonjwa cha hospitali ya rufaa ya Mkoa Sekou Toure na kwamba rufaa 4775 zimefanyika na Jumla ya Milioni 14.4 zimechangwa kwenye akaunti ya Taifa.
Meneja wa kanda wa shirika la Pathfinder Charles Kato amesema kuwa wanayo furaha kukabidhi majukumu ya utekelezaji wa usafiri wa dharula kwa wajawazito, waliojifungua pamoja na watoto na kwamba wataendelea kushirikiana na Serikali katika kushauri masuala mbalimbali.
Vilevile, Meneja huyo amebainisha kwamba wahisani wote awali walijipanga kuihudumia mikoa yote ya Tanzania hadi 2027 kwa kushirikiana na Serikali na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza ifikapo Oktoba 2024 wahakikishe wamefika kote na kukabidhi majukumu kwa watendaji wa Serikali ili kujenga tabia ya kujitegemea.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.