RC MAKALLA AMEWATAKA WANANCHI KULINDA VIFAA VYA MRADI WA SGR
*Aomba ushirikiano katika kuwaletea maendeleo wananchi*
*Aipongeza Kwimba kwa mafanikio, aiangazia michezo*
*Asisitiza kudumishwa kwa Usalama kwa wananchi*
*Awataka viongozi kutoa elimu dhidi ya madhara ya imani za Kishirikina*
*Ana imani kubwa na nidhamu kazini kama dira ya Maendeleo*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. CPA Amos Makalla amempongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutekeleza miradi ya kimkakati nchini hususani mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na amewataka wananchi kulinda Miundombinu hiyo kizalendo ili ufikie adhama ya kukuza uchumi wa nchi.
Akizungumza na viongozi, watendaji na makundi mbalimbali leo tarehe 02 Juni, 2023 kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba Mhe. Makala amesema uchumi wa nchi utakua zaidi kupitia Miradi ya kimkakati hivyo ni lazima wananchi wawe wazalendo kuilinda kusiwe na upotevu wa vifaa wakati wa utekelezaji.
"Tukiruhusu wizi wa vifaa na mafuta kwenye miradi yetu tunajiibia wenyewe na tunajichelewesha kupata maendeleo, nawaomba wana Kwimba tulinde mradi wa SGR na tuhakikishe vifaa kwenye kambi ya Ujenzi iliyopo hapa haviibiwi kwani mradi huo ukikamilika tutasafirisha Pamba kwa haraka sana na tutakuwa kiuchumi." CPA Makalla.
Aidha, ametumia wasaa huo kuomba ushirikiano kwa viongozi na watumishi wote huku wakitanguliza nidhamu mahala pa kazi ili kwa pamoja waweze kumsaidia Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kuwaletea maendeleo wananchi katika kila sekta hususani za kilimo, uvuvi, uchimbaji madini na biashara.
Vilevile, ameipongeza wilaya hiyo kwa mafanikio na maendeleo makubwa waliyofikia tofauti na siku za nyuma na kwamba amewataka kuendelea kudumisha amani ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na uhuru wa kufanya kazi za maendeleo na kuacha tabia za kufanya ramli chonganishi.
"Inashangaza kuona Chuo cha michezo nchini kipo hapa Kwimba kinaitwa Malya ila Mkoa huu hauna timu kwenye ligi kuu, ni lazima tufanye mageuzi kwenye michezo ili chuo hiki kitunufaishe kwanza sisi wenyewe na turudishe furaha kwa wananchi wa Mwanza", Mhe. Makalla akizungumzia Michezo.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba Mhe. Ng'wilabuzu Ludigija amesema wananchi wa wilaya hiyo wanaendelea na uzalishaji ambapo kwa sasa wapo kwenye mavuno ya Pamba, Mahindi na Mpunga lakini vilevile wanalima choroko kwa amani kutokana na kazi nzuri inayofanya na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na Sungusungu.
"Tunaendelea kufanya mikutano kwa wananchi tukiwakumbusha kutunza chakula kwa ajili ya siku za baadae kwani kwa kuzingatia historia ya msimu uliopita hawakufanikisha mavuno mengi hivyo ni lazima kuweka akiba na tunahakikisha pembejeo za kilimo zinawafikia wakulima wetu kwa wakati," amesema Mhe. Ludigija
Ameongeza kuwa kwa mwaka wa fedha uliopita Halmashauri hiyo ilitengewa Bilioni 20 kutekeleza miradi ya maendeleo na hadi sasa wamepokea zaidi ya fedha hizo lakini vilevile Halmashauri hiyo inayotegemea kukusanya kupitia kilimo wameshakusanya Bilioni 3.2 ambapo ni sawa na 97% ya makadirio.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.