*RC Malima awataka Wamachinga kufanya biashara kwenye maeneo rasmi*
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ametoa rai kwa Wafanyabiasha wadogo (Machinga) Mkoani humo kufanya biashara zao kwenye maeneo rasmi ili kuweka mazingira ya miji kuwa nadhifu yatakayovutia wageni hata kusaidia ukuaji wa Sekta ya Utalii.
Mhe. Malima amesema hayo leo jumanne disemba 20, 2022 wakati wa Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa kilichohudhuriwa na viongozi wa kundi hilo na akaongeza kuwa endapo watakuwa na changamoto kwenye shughuli zao wanapaswa kuwasilisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya utatuzi.
"Natamani kila mwananchi wa nchi hii ambaye anaishi Mkoani Mwanza astawi kiuchumi kama malengo ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan alivyojipambanua katika falsafa ya uongozi wake na katika kuyafikia haya ni lazima kila mmoja afuate taratibu za kisekta." Malima.
Vilevile, ametoa wito kwa Halmashauri Mkoani humo kuwa na mipango thabiti ya Ukusanyaji wa mapato ikienda sambamba na uwezeshi wa makundi yote ya Wafanyabiasha kwa kuhakikisha huduma zote za kijamii zinapatikana.
Hata hivyo, ametoa wito kwa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Mjini Mwanza ( MWAUWASA), Wakala wa Maji Mijini na Vijijini (RUWASA) na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Sengerema (SEUWASA) kutekeleza miradi ya Maji kwa ufanisi ili kuongeza Mtandao wa huduma ya Maji kwa wananchi.
Halikadhalika, Mhe. Malima amewahimiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege kukamilisha Ujenzi wa Jengo la Kisasa la abiria kwenye uwanja wa Ndege wa Mwanza ili kuweka mazingira rafiki kwa wageni kufika ambapo amebainisha kuwa uwepo wa Miundombinu hiyo itasaidia kukuza sekta ya Utalii kwa wageni kutalii kwenye hifadhi za kanda ya Ziwa wakitumia uwanja huo.
Akiwasilisha taarifa ya Timu iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa kufuatilia Ukarabati wa Kivuko cha MV Misungwi, Katibu wa Kamati hiyo Chagu Ng'homa amesema TEMESA na Songoro Marine waliingia Mikataba miwili ya ukarabati wa Kivuko cha MV Misungwi na kukamilisha kufikia Machi 20, 2023.
Kamati hiyo imebaini kuwa Mkandarasi anao uwezo wa kukamilisha ukarabati huo ndani ya muda kwani tayari ameshaagiza Injini Mpya na vifaa vingine nchini Korea ambavyo kwa pamoja vitawasili nchini ifikapo Januari 30, 2023 lakini imeshauri kuwe na ufuatiliaji wa karibu kwenye karakana hiyo ili kusukuma utekelezaji.
Kwa upande wa Sekta ya elimu Mkuu huyo wa Mkoa ametaka kuwepo na jitihada za makusudi za kuwepo na uwiano mzuri wa walimu hasa maeneo ya nje ya mji ambako wengi hawapendi kwenda kufanya kazi.
Amesema Serikali imeweka mazingira rafiki kwa walimu waweze kufanya kazi vizuri ikiwemo kuwapatia nyumba bora lakin bado idadi kubwa wamerundikana mjini.
"Mkoa wa Mwanza umepatiwa zaidi ya Shs Bilioni 19 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa kwenye Halmashauri zote za Mkoa huu na tuna uhakika wanafunzi wote waliofaulu kwa kidato cha kwanza mwakani watasoma kwenye mazingira bora" Afisa Elimu Mkoa Martin Nkwabi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.