RC MTANDA AMPOKEA NAIBU WAZIRI WA MAJI MWANZA
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo Julai 24, 2024 Ofisini kwake amempokea na kufanya mazungumzo mafupi na Naibu Waziri wa Wizara ya Maji Mhandisi Kundo Mathew aliyefika mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku tatu.
Mhe. Mkuu wa Mkoa ametumia wasaa huo kuipongeza Wizara hiyo kwa juhudi za kupunguza adha ya maji kwa wananchi kwa kutekeleza miradi kadhaa huku akitolea mfano wa kazi nzuri inayofanywa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA).
"Tuna chanzo kipya cha Butimba na kwasasa changamoto yetu ni kwenye usambazaji, naamini mkandarasi yupo kazini kwa ajili ya upanuzi wa usambazaji kutoka kwenye chanzo cha Butimba kupitia fedha zaidi ya Bilioni 49 zilizotolewa na Shirika la maendeleo la ufaransa." Mkuu wa Mkoa.
Aidha, Mhe. Mtanda ametoa wito MWAUWASA kuhakikisha wanasimamia ulipwaji wa fedha zilizobaki kwenye chanzo cha mradi wa maji wa Butimba na ikiwezekana waongeze pampu ili kuongeza uzalishaji wa maji.
Vilevile, amewasihi kuendelea kusimamia miradi ya usafi wa mazingira na maji taka ili kuwahakikishia afya njema wananchi wa Mkoa wa Mwanza ambao wana matumaini makubwa na huduma bora za kijamii zinazotekelezwa na Serikali ya awamu ya sita.
"Kazi yoyote ni ibada na ibada njema ni kufanya kitu kwa utimilifu wake hivyo naamini watumishi wa sekta ya maji wataendelea kujituma ili kuhakikisha wanawatumikia wananchi." Mkuu wa Mkoa.
Naye, Naibu waziri Mathew amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa Wizara hiyo itaendelea kupokea na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kwamba watahakikisha usambazaji maji vijijini unafikiwa kwa asilimia 85 ili kuinua uchumi wa wananchi.
"Sekta ya maji imebadilika sana nasi kama Wizara tunaendelea kufanya ufuatiliaji wa kina kutokana na msukumo wa Mhe. Rais ambaye amedhamiria kumtua mama ndoo kichwani iliyopelekea kupatikana kwa sheria namba tano ya 2019 ambayo imewazaa RUWASA" Mhe. Waziri.
Aidha, amewataka Mamlaka za maji mkoani humo kutengeneza mfumo mzuri wa kupata taarifa zinazohusu changamoto za maji kutoka ngazi za vitongoji hadi juu ili wawafikie na kurekebisha kwa haraka.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.