Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amempa mkandarasi anayejenga Shule ya Sekondari Nela wilayani Kwimba siku 10 kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya madarasa nane pamoja na matundu 16 ya vyoo ili kuwezesha wanafunzi kuanza masomo.

Agizo hilo limetolewa mapema leo Januari 16, 2026 wakati Mhe. Mtanda alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kijiji cha Nela ambapo alikagua ujenzi wa shule hiyo unaotekelezwa kwa gharama ya shilingi milioni 267.050 na Mkandarasi wa Kampuni ya Mairo Group of Companies, na kubaini kuwepo kwa ucheleweshaji wa utekelezaji wa mradi.

Katika kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati Mhe. Mtanda amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kufanya tathmini ya kazi zote zilizotekelezwa hadi sasa na kuhakikisha anampatia mzabuni mwenye uwezo wa kukamilisha ujenzi uliobaki kwa kutumia fedha ambazo bado mkandarasi wa awali hajalipwa.

Aidha, Mkuu wa Mkoa amesisitiza umuhimu wa kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi huo kwa kufanya kazi usiku na mchana akibainisha kuwa tarehe ya Februari 28, 2026 ambayo awali ilipangwa kuwa mwisho wa mradi ni mbali na inaweza kuwanyima wanafunzi fursa ya kuanza masomo kwa wakati.

Halikadhalika, Mhe. Mtanda ameagiza Ofisi ya TAKUKURU wilayani Kwimba kufuatilia kwa kina mwenendo wa zabuni ya ujenzi wa shule hiyo pamoja na utendaji wa Idara ya Manunuzi kwa ujumla na kuwasilisha taarifa ya uchunguzi huo.

Wakati huo huo, Katibu Tawala wa Mkoa ameagizwa kumwondoa Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi katika halmashauri hiyo na kumhamishia mkoani kufuatia tuhuma za uzembe na ukiukwaji wa taratibu za manunuzi.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.