Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa Chemba ya wafanyabiashara nchini TCCIA kuzingatia sera za biashara na viwanda pia kuzingatia kilimo endelevu kinachotumia teknolojia zinazohimili mabadiliko ya tabianchi ili kuongeza tija katika kazi zao.
Mhe. Mtanda ametoa wito huo leo jumanne tarehe 02 Septemba, 2025 wakati akifungua maonesho ya 20 ya Biashara ya Afrika Mashariki katika Uwanja wa Nyamagana.
Amesema kadri siku zinavyokwenda jamii imekua ikiongezeka na kusababisha uharibifu wa mazingira hivyo chemba hiyo ina wajibu wa kutoa elimu kwa jamii kufanya shughuli za Uvuvi, biashara na kilimo cha kisasa pasipo kuharibu mazingira ili kuwa na jamii endelevu.
Aidha, amesema kuwa Serikali inaendelea kuwahimiza na kuwawezesha Wafanyabiashara kuchangamkia fursa zilizopo katika soko la Afrika Mashariki katika Nchi za Kenya, Uganda, Congo, Tanzanıa, Kusini, Burundi, Rwanda na Sudan.
“Maonesho haya ni jukwaa la kuimarisha mahusiano ya kibiashara kwa kubadilishana ujuzi, uzoefu na mazingira ya biashara. Pia yanatoa fursa kwa kampuni za ndani kujifunza Mbinu za kukuza biashara ya nje kwa kutumia masoko ya kimataifa kama SADC, AFCFTA, India, AGOA na China” Mhe. Mtanda.
Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara Taifa Bwana Vincent Minja amesema kuanzia mwaka 2026 wamejipanga kuboresha maonesho hayo yakijumuisha wadau wengi zaidi kutoka nchi zote wanachama ili kuyapa hadhi ya siku za nyuma.
Naye, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mwanza Ndugu Gabriel Chacha amesema maonesho hayo yanaongeza mzunguko wa kifedha ndani ya nchi na kusaidia kubadilishana teknolojia kwa wafanyabiashara kutoka nchi wanachama.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.