RC MTANDA AWATAKA SENGEREMA DC KWENDA KUJIFUNZA TARIME DC UENDESHAJI MIRADI YA CSR
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema kwenda kutembelea na kujifunza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime Mkoani Mara kuhusu upokeaji na uendeshaji wa fedha za Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR) zinazotolewa na Migodi ya Dhahabu ili kuleta ufanisi na manufaa kwa wananchi wanaozunguka mgodi wa Sotta.
Mkuu wa Mkoa ametoa wito huo mchana wa leo Novemba 25,2024 wakati wa hafla ya kukabidhi Madawati 1131 na samani mbalimbali zenye thamani ya jumla ya Tshs. Milioni 93.8 vilivyotolewa na Mgodi wa Sotta mining Co. Ltd uliopo Wilayani Sengerema.
Akizungumza na wananchi baada ya makabidhiano hayo Mhe. Mtanda amewashukuru viongozi wa mgodi huo kwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuwaondoa watoto kwenye adha ya kusongamana na kukaa chini kwa kuwapatia samani hizo.
Aidha, ameitaka Halmashauri hiyo kutoa elimu kwa vijiji ili wajiandae na kuunda kamati za Uwajibikaji wa Fedha za Kampuni kwa jamii (CSR) ili uzalishaji utapoanza waweze kukidhi kanuni zilizopitishwa na tume pamoja na wizara ya Madini.
"Na niwashauri tu muende mkajifunze kule Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Musoma na Butiama wao wameanza zamani wana uelewa wa kutosha kuhusu CSR na mimi nilikuwa huko kwa hiyo ninaelewa".
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema Ndugu Binuru Shekidele amewashukuru na kusema mgodi umewapunguzia adha na kwamba kwa msaada huo watabaki na upungufu wa madawati elfu 12 tu kwa shule za msingi.
Kwa upande wake Afisa Mahusiano kutoka Kampuni ya Mgodi wa Sota Bi. Habiba Said Amesema madawati na samani hizo zimetolewa ikiwa na lengo la kuimarisha mahusiano kwa kuwa bado mgodi huo haujaanza kufanya kazi na wanatarajia kuanza kutoa CSR pindi mgodi huo utakapoanza uzalishaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.