Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe,Mhandisi Robert Gabriel amezikumbusha Halmashauri zote Mkoani humo kuweka kipaumbele maeneo ya ardhi kwa ajili ya Wawekezaji.
Mkuu wa Mkoa amesema hayo wakati wa kikao cha Baraza la Biashara la Mkoa wa Mwanza,amesema Mkoa huo una fursa nyingi za biashara na ardhi ndiyo mtaji wa msingi katika suala la uwekezaji.
"Naagiza maeneo yote yawe yamepimwa ili anapofika mwekezaji kusiwepo na ubabaishaji wa kuanza kumzururisha ili kujenga ushawishi wa kupata chochote,tutapoteza kuwapata wenye nia ya kuwekeza"
Gabriel amesema pia eneo kubwa la Mkoa wa Mwanza ni maji lenye Ziwa Victoria hivyo tunapozungumzia Uchumi wa bluu tutambue fursa zilizopo Ziwani humo likiwemo ufungaji wa Samaki kwa njia ya Vizimba.
"Hizi ni fursa ambazo tuna wajibu wa kuzisimamia na kuweka mazingira mazuri kwa Mwananchi ili kukuza Uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa Kwa ujumla."
Katika kikao hicho Mkuu huyo wa Mkoa amekiri mgogoro wa kimataifa kwa Mataifa ya Ulaya,Urusi na Ukraine imechangia Uchumi kunyumba na kuchangia bidhaa kupanda bei hasa ya nishati ya Mafuta,amewataka Wafanyabiashara kujenga mshikamano wa pamoja kwa kipindi hiki cha mpito na siyo kutumia nafasi hiyo kumtwisha mzigo mwananchi kutokana na upandaji bei ya bidhaa.
Kikao hicho cha Baraza la Biashara la Mkoa wa Mwanza wamezungumzia na kuweka mikakati mbalimbali ya kukuza Uchumi wa Mkoa huo.
Baraza la Biashara la Mkoa wa Mwanza linawajumuisha Wafanyabishara wakubwa wenye Viwanda,Taasisi za Serikali na binafsi, na wajumbe wa
Mabaraza ya Biashara kutoka Wilaya
zote za Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.