Serikali katika kuhakikisha inaboresha zao la Pamba na kumuwekea mazingira rafiki Mkulima imeongeza bajeti ya Utafiti kwa Wataalamu wa kilimo kutoka Shs Bilioni 11.7 hadi kufikia bilioni 40 na bajeti ya Mbegu ikitengewa Shs Bilioni 43.
Akizungumza leo wakati wa ugawaji zana za kilimo na usafiri zenye lengo la uboreshaji wa zao la Pamba kwenye Kituo cha Utafiti wa kilimo TARI kilichopo Wilayani Misungwi,Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.Anthony Mavunde amesema bajeti hiyo ya utafiti imelenga pia kuboresha Maabara zote za udongo ili kumuhakikishia Mkulima uhakika wa kilimo chake na kupata mazao bora.
Amesema Serikali hii chini ya uongozi wake Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuleta mageuzi ya kweli kwenye Sekta hiyo ikitenga bajeti ya Shs Bilioni 361 ambazo zimelenga kuleta mageuzi chanya sehemu mbalimbali ukiwemo mkakati kamambe wa kuwapa ajira vijana.
"Tumeanza mradi huo kwa Vijana kuwawekea mazingira mwafaka ya kilimo kwa kuanza na Mikoa 2 ya Dodoma sehemu za Chamwino na Mbeya huko Chunya na kutenga jumla ya hekari 69000 lengo likiwa kuwafikia Vijana milioni 3 kabla ya mwaka 2030 wawe na ajira kupitia Sekta hiyo" Mhe.Mavunde
Amewakumbusha Wataalamu wa kilimo kwenye Kituo cha Utafiti Ukiriguru kuongeza ubunifu zaidi ili Mkulima azidi kupata tija kwenye mazao yake hasa Pamba ambayo ndiyo zao lenye nguvu kwenye soko la Dunia.
Ameongeza kuwa Maafisa Ugani katika kuwawekea mazingira bora ya kutoa elimu kwa mkulima wameongezewa bajeti yao kutoka Shs milioni 600 na sasa ni Shs Bilioni 15 huku wakisambaziwa jumla ya Pikipiki 7,604 zitakazo rahisisha mazingira ya kazi zao.
Akitoa taarifa za Mkoa wa Mwanza kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa huo Bw. Balandya Elikana,Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji Emil Kasagara amesema Mkoa wa Mwanza msimu wa kilimo 2022/2023 unatarajia kulima zaidi ya hekta 67000 za Pamba zenye makisio ya mavuno ya Tani 56,000.
Naibu Waziri Mavunde amegawa zana za kilimo zikiwa ni baadhi kutoka kwenye mradi wa BEYOND COTTON unaofadhiliwa na Serikali ya Brazil zikiwemo mashine za kuandaa shamba 3,zana za kupandia 600, na zana za kupalilia 3 pamoja na Pikipiki 3kwa ajili ya Maafisa Ugani.
Serikali ya Tanzania Julai mwaka huu hadi Disemba 2023 imeingia rasmi mkataba na Nchi ya Brazil wa kuendeleza zao la Pamba pamoja na chakula na lishe,Taifa hilo kutoka Amerika ya Kusini likitoa Dola za Kimarekani 629,000 kugharamia mradi huo ujulikanao kama BEYOND COTTON.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.