Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo tarehe 29 Januari, 2026 amekagua na kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa shule mpya ya Sekondari kwa mfumo wa ghorofa mtaa wa Kasota, kata ya Mhandu Wilayani Nyamagana.

Akizungumza na wananchi kwenye hafla hiyo Mhe. Mtanda ameipongeza serikali kwa kutoa fedha na Uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza kwa maendeleo ya kasi katika sekta ya elimu na kwamba kuanzia mwaka 2021 hadi sasa kumekua na ongezeko la shule za sekondari 58 kutokana na juhudi zao.

Aidha, ameiagiza Halmashauri hiyo kutoa fedha Tshs. Milioni 200 na kusimamia kwa kasi ukamilishaji wa ujenzi wa shule hiyo hadi kufikia mwezi desemba mwaka huu ili mapema mwezi januari mwakani wanafunzi waanze kusoma katika madarasa ya shule hiyo mpya na kusaidia kuondoa msongamano kwenye shule mama.

Halikadhalika, amewataka MWAUWASA na TANESCO kuhakikisha wanafanikisha huduma za Maji na Umeme kwenye shule hiyo mpya ili kuongeza kasi ya ujenzi na pia kwenda sambamba na ujenzi wa miundombinu mara ujenzi utakapokamilika wanafunzi waanze kuyatumia bila kusubiri huduma za msingi.

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Makilagi amesema shule hiyo itakapokamilika itachukua wanafunzi 1620 na itasaidia Kata hiyo kuwa na shule mbili za sekondari na kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani pamoja na kupunguza umbali kwa wanafunzi kwenda Mhandu sekondari.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Mhandu Warioba Marato amesema Mwezi Juni 2025 Serikali ilitoa Tshs. Milioni 584.2 kwa ajili ya kujenga Shule ya sekondari ya kawaida katika kata hiyo lakini kutokana na ongezeko la wanafunzi kuwa kubwa halmashauri iliamua kujenga kwa mfumo wa ghorofa.

Mwalimu Marato ameongeza kuwa mnamo Mei 2025 kibali kilitolewa na kuanza rasmi kwa ujenzi wa shule hiyo kwa mfumo wa ghorofa katika mtaa wa Kasota na hadi kukamilika wanahitaji nyongeza ya Tshs. Bilioni 1.56 ambapo sasa ujenzi umefikia 45%.

Halmashauri ya wilaya ya Nyamagana kwa mwaka 2026 wanafunzi 13609 wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha kwanza na mpaka sasa wanafunzi 10195 wameripoti shuleni.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.