Katika kuimarisha na kurahisisha shughuli za ukusanyaji wa mapato nchini, Mamlaka ya Mapato (TRA) imeanzisha Mfumo jumuishi wa Kodi za ndani ambao unatarajiwa kuanza kutumika ifikapo Februari 09, 2026 kote nchini na TRA Mwanza inatoa mafunzo kwa wafanyabiashara ili kujengewa uwezo.

Akifungua Mafunzo hayo katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana ameipongeza Mamlaka hiyo kuingia kwenye dunia ya kidigiti ambapo itaongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato kwani mfanyabiashara hatokwenda katika ofisi za TRA kufuata huduma.

“Nawapongeza sana TRA kwa kuja na wazo ambalo linaenda sambamba na dira ya serikali ya kutumia TEHAMA kusogeza na kurahisisha huduma za kikodi kwa wafanyabishara nchini.” Amesema Katibu Tawala.

Aidha, amewataka TRA kuhakikisha kabla ya kutekeleza mfumo huo wawafikie wafanyabiara kwa umakini na kuwapitisha katika moduli zote ili kusiwe na changamoto zitokanazo na ugumu wa mfumo.

“Ninawashukuru wafanyabiashara wa Mwanza kwa kuwa walipa kodi wazuri na natoa wito kwenu tuendelee hivyohivyo kwani kodi ndizo zinaipa fursa serikali kufanya miradi ya maendeleo ya jamii kama tulivyoona Daraja la JPM pamoja na Meli ya Kisasa vilivyotekelezwa na kodi zetu na sasa zinakwenda kuinua uchumi wetu.” Ndugu Balandya.

Akitoa utangulizi, Meneja wa TRA Mkoa wa Mwanza Bw. Faustine Mdesa amesema Kikao hicho cha siku tatu ni mahususi kwa wafanyabiashara kupatiwa mafunzo ya mfumo Jumuishi wa Kodi za ndani ambao unatarajiwa kuanza kufanya kazi ifikapo februari 28, 2026 kote nchini.

Amebainisha kuwa wafanyabiashara hao watapitishwa kwenye moduli 17 za zinazojumuisha namna ya Usajili, Ulipaji na ufuatiliaji wa masuala ya kikodi ambayo kwa ujumla yatampa fursa mfanyabiashara kumaliza masuala yote ya kikodi ndani ya mfumo pasipo kwenda kwenye ofisi za TRA.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.