Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amesema uimarishwaji wa matumizi ya mifumo ya Kielektroniki imekuwa na manufaa makubwa, imeongeza tija na uwajibikaji katika utendaji wa shughuli za Serikali na taasisi zake, pamoja na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Katibu Tawala ameyasema hayo leo Julai 23, 2025 wakati akifungua mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa taarifa za utekelezaji wa programu za maboresho nchini yaliyofanyika jijiji Mwanza na kujumuisha Mikoa mitatu ya Mwanza, Shinyanga na Geita.
Aidha, Katibu Tawala amesema mifumo imepunguza gharama na kuongeza upatikanaji wa taarif na kwa msingi huo, ili kurahisisha uwasilishaji wa Taarifa za Utekelezaji wa Mkakati, Serikali imeandaa mfumo wa taarifa za utekelezaji wa programu za maboresho nchini ukiwemo mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa awamu ya nne.
“Serikali ingependa kuona kuwa rushwa inatokomezwa katika utoaji huduma ili kuiwezesha kutekeleza ipasavyo jukumu lake la Kikatiba la uwepo wa Ustawi wa Wananchi kama lilivyotamkwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Ibara ya 8 (1) (b).)”.
Sambamba na hayo Bw. Balandya amesema ni wajibu wa kila taasisi kuhakikisha kuwa utekelezaji wa mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa awamu ya nne unasimamiwa na taarifa za utekelezaji zinawasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi kwa wakati.
“Hivyo, mafunzo ya matumizi ya mfumo huu ambayo yatachukua siku mbili ni ya msingi kwetu sote katika kuhakikisha kuwa taarifa husika zinachakatwa na kuwasilishwa kwa wakati”.
Ndugu Balandya ameishukuru Ofisi ya Rais, Ikulu kwa kuona umuhimu wa kutoa mafunzo hayo kwa mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Geita na amewasisitizia washiriki kwamba, baada ya mafunzo hayo wautumie kikamilifu mfumo huo kuchakata na kuwasilisha taarifa za utekelezaji kwa wakati.
Tukumbuke kuwa taarifa za utekelezaji wa mipango kazi zina mchango katika maamuzi mbalimbali ya msingi ya kitaifa. Hivyo suala hili tulipe umuhimu wake ili matokeo tarajiwa ya utekelezaji wa Mkakati wa Taifa dhidi ya rushwa yaweze kufikiwa. Ameongeza Katibu Tawala.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.