Mkuu wa Mkoani wa Mwanza Mheshimiwa Adam Malima, amewataka wakulima kuendelea kufuata kanuni bora za kilimo wanapolima mazao ya chakula na biashara ili kuongeza tija ya uzalishaji.
Akizungumza leo Agosti 4, 2022 wakati akifungua maonesho ya kilimo na sherehe za wakulima nane nane kwa Kanda ya Ziwa Magharibi yanayofanyika katika Viwanja vya Nyamhongolo Manispaa ya Ilemela Mkoani Mwanza, Mheshimiwa Malima amesema Sekta za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi ndizo zinazoajiri nguvu kazi kubwa hapa nchini kuliko sekta zingine ambapo kati ya asilimia 63 hadi 65 imeajiriwa na hutegemea kupata riziki katika Sekta ya Kilimo.
"Hivyo uwekezaji katika Sekta ya Kilimo itasaidia sana kuimarisha usalama wa chakula, kuongeza pato la taifa na kupunguza umaskini katika Kanda ya Ziwa Magharibi inayojumuisha Mikoa ya Mwanza, Geita na Kagera pamoja na taifa kwa ujumla ambalo ndilo lengo la Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshiwa Samia Suluhu Hassan," amesema Mhe.Malima.
" Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anashirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili nchi yetu iendelee kukua kiuchumi kufikia maendeleo ya viwanda ambapo malighafi za viwanda hivi viweze kutokana na sekta ya kilimo ikiweo uvuvi na mifugo,"amefafanua Mheshimiwa Malima.
Mheshimiwa Malima amesema kauli mbiu ya maadhimisho ya nane nane mwaka huu isemayo 'Ajenda 10/30: Kilimo ni biashara ,Shiriki kuhesabiwa kwa Mipamgo Bora ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 'inawajulisha wananchi na wakulima kwamba Serikali inalenga kuona Sekta ya Kilimo inakuwa kwa asilimia 10 kufikia mwaka 2030.
"Fursa zilizopo Kanda ya Ziwa Magharibi zinazoweza kuchangia katika ukuaji wa Sekta ya Kilimo ni pamoja na uwepo wa Ziwa Victoria linaloweza kutumika katika kilimo cha umwagiliaji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi hasa ukame pamoja na ufugaji wa samaki hasa kwa njia ya vizimba.
" Fursa nyingine katika kutekeleza kauli mbiu ya mwaka huu hasa Ajenda 10/30 Kilimo ni biashara ni kwamba Kanda ya Ziwa Magharibi ni Kituo katika nchi za Maziwa Makuu, Afrika Mashariki, Mikoa na Kanda za jirani na katika nchi za Maziwa Makuu pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki hivyo ni rahisi kuuza mazao ya sekta ya kilimo katika nchi za Kenya, Uganda, Burundi na Rwanda," Mhe. Malima amewaambia Wakulima.
Aidha amewataka wakulima kunufaika na uwepo wa Taasisi za fedha zaidi ya 24 zinazofanya kazi katika Kanda hiyo kwa kukopa mitaji itakayowawezesha kuwekeza katika sekta ya kilimo huku akiwasisitiza wananchi wote kushiriki katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufayika Agosti 23, 2022 ili Serikali ipate takwimu zitakazoiwezesha kupanga Mipamgo ya Maendeleo.
Vilevile amewataka wananchi wa Kanda ya Ziwa Magharibi kujikinga na ugonjwa wa UVIKO 19 kwa kupata chanjo dhidi ya ugonjwa huo ili wafanye shughuli za kiuchumi bila kikwazo.
Awali akitoa taarifa ya maonesho hayo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Maonesho ya Kilimo na Sherehe za Wakulima Nane Nane 2022, Kanda ya Ziwa Magharibi, Emil Kasagara, amesema maonesho hayo ambayo yalianza rasmi kwa kanda hiyo mwaka 2017 yamekuwa yakikumbwa na chamgamoto mbalimbali hususani ukosefu wa Miundombinu ya kudumu hali hiyo huongeza gharama za uratibu hasa wakati wa ujenzi au ukarabati wa miundombinu Mara kwa Mara.
Akizungumzia mafanikio ya Maonesho hayo,2022, Kasagara amesema hadi Agosti 3,2022 idadi ya washiriki walikuwa zaidi ya 228 ikijumuisha Mamlaka za Serikali za Mitaa wenye shughuli kubwa na za kati, Taasisi za fedha elimu,afya, kampuni za zana za kilimo,usambazaji pembejeo vinywaji na kampuni za mawasiliano.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwa nza Bwana Balandya Elikana amemshukuru Mhe.Rais kwa kumchagua kuja kuendeleza maendeleo ya Mkoa wa Mwanza na kuwaomba wananchi kuonyesha ushirikiano katika kuleta maendeleo ya Mkoa wa Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.