VIFUNGASHIO VYA PLASTIKI NI KIZUIZI CHA AFUA ZA LISHE BORA
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza ndugu Balandya Elikana ametoa wito kwa Viongozi wa dini na asasi za kiraia mkoani humo kushirikiana na serikali kuelimisha jamii juu ya madhara ya vifungashio vya plastiki kwenye lishe bora.
Ametoa wito huo leo tarehe 06 Februari, 2025 wakati akifungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe ngazi ya Mkoa kwa kipindi cha Mwezi Oktoba- Desemba, 2024 uliowakutanisha wataalamu na wadau mbalimbali.
Amesema, kiafya kuna madhara makubwa sana kula chakula kilichohifadhiwa kwenye kifungashio cha plastiki mathalani maziwa ya ng'ombe na chakula cha moto kinachowekwa kwenye mifuko hivyo jamii ni ielimishwe kuacha tabia hiyo mara moja.
Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Jesca Lebba alifafanua kuwa suala la lishe ni mtambuka na kila mmoja anapaswa kushirikiana na Serikali kutekeleza afua za lishe ikiwemo uhifadhi wa chakula unaokubalika ili kulinda virutubisho.
Aidha, ametoa wito kwa halmashauri kupanga bajeti na kuitekeleza ili kuwezesha watoto wa shule kupata chakula wakati wa masomo na kushirikiana na wadau katika kuhamasisha upandaji wa miti ya matunda shuleni.
Ameongeza kuwa wajawazito wanapohudhuria kliniki wanapewa dawa za fefo zenye mchanganyiko wa virutubisho vya madini chuma na foliki asidi kwa ajili ya kuwaongezea damu hivyo hawana sababu ya kutumia udongo ambao una athari kiafya.
Kwa upande wa wadau hao wameshauri Kamati ya Lishe Mkoa kufanya juhudi za binafsi kufuatilia biashara ya Udongo unaotumiwa na wajawazito (Pemba) ambao una athari kiafya kwani unamuathiri mtumiaji na mtoto wa tumboni.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.