Wananchi na Viongozi wa Mkoa wa Mwanza wameungana kufanya dua na sala maalum kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kumuombea afya njema, hekima na nguvu ili aendelee kuliongoza Taifa kwa amani na umoja.

Hafla ya dua na sala imefanyika katika Viwanja vya Rock City Mall wilayani Ilemela ikiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda kwa kushirikisha madhehebu ya dini za Kiislamu na Kikristo chini ya uratibu wa Kamati ya Amani ya Mkoa.

Akizungumza katika hafla hiyo Mhe. Mtanda amesema Mkoa wa Mwanza umeamua kumuombea Rais dua na sala maalum kama ishara ya mshikamano na kumuunga mkono katika jukumu zito la kuliongoza Taifa.

Amesema uongozi wa Rais Samia umeendelea kudumisha amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa hususani katika nyakati za changamoto hatua ambayo imeongeza imani na matumaini kwa wananchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana Mhe. Amina Kakilagi amesema wananchi wa Mwanza wataendelea kumuunga mkono Rais kwa kufanya kazi kwa bidii, kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kulinda amani iliyopo.

Katika kuadhimisha tukio hilo, wananchi pia walishiriki zoezi la upandaji miti zaidi ya 16,000 kama sehemu ya jitihada za kuhifadhi mazingira. Hafla hiyo pia ilihusisha kula chakula cha pamoja kati ya Mkuu wa Mkoa na watoto zaidi ya 200 wanaolelewa katika makao maalum kutoka vituo vya hisani vikiwemo Fone Risto, FKT Foundation na Watoto wa Afrika.


Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.