Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) imesema viwanja vingi vya ndege vimeshindwa kupata hati miliki kutokana na wananchi kuvamia maeneo hayo na kusababisha migogoro ambayo ipo kwenye vyombo vya uamuzi.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mtendaji Mkuu wa TAA, Richard Mayongela wakati akimwelezea Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Isack Kamwelwe wakati wa majumuisho ya Waziri mkoani Mwanza ambapo alisema kati ya viwanja vyote 58, vilivyo na hati ni 8.
Alisema kutokana na hali hiyo TAA imeanza kushughulikia migogoro hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambapo hadi sasa viwanja vingine vinne vipo katika hatua ya mwisho kupewa hati mmiliki na kufikisha idadi ya 12 kati ya 58.
Mayongela alisema mkakati wao ni kuhakikisha viwanja vyote nchini vinakuwa na hati miliki na ikiwezekana kuwekewa uzio ili kuepusha tena migogoro ya uvamizi.
“Nitumie fursa hii kuwasilisha kwako Mhe.Waziri changamoto zinazotukabili TAA, kwanza tumezoea kuitwa mamlaka lakini hatujapata nguvu hiyo bali kisheria tunatambulika kama wakala, sasa kutokana na hali hiyo tunashindwa kuwa na mamlaka kamili ya maamuzi, ikiwa tutapata mamlaka hayo tutaongeza utendaji Zaidi,”alisema Mayongela.
Aidha aliongeza kuwa,Mhe Waziri akiwa unapitia nakala ofisini kwake akifika kwenye kipengele hicho wanamuomba amalizie kipengele kadhaa ili wawe na mamlaka kamili, jambo lingine ni maslahi kwa wafanyakazi ni madogo mno kwani muda mrefu hayajaboreshwa jambo ambalo linasababisha hata hali ya utendaji kwa watumishi kupungua lakini wanamshukuru Rais Dk. John Magufuli ameonyesha dhamira ya dhati katika kuboresha miundombinu ya viwanja vya ndege.
“Lipo jambo la kuboresha baadhi ya viwanja vyetu ili kuwa na vya kimataifa kwani hata ndege kubwa ya dreamline iliyokuja hivi karibuni inatua katika viwnaja vichache kama Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza, hivyo inatubidi kuendelea kuboresha na kuwa na hadhi ya kimataifa, pale Dodoma ambapo ndio makao makuu, tunatarajia kufanya maboresho ya uwanja wa Msalato ili kuwa wa kimataifa,”alisema Kamwelwe.
Mayongela alimuomba Waziri Kamwele kusaidia kukamilika mradi wa ujenzi wa uwanja wa Songwe ambao umechukua muda mrefu ili huduma ziweze kuendelea huku akitoa wito kwa Watanzania wote kuitunza miundombinu inayojengwa kwani fedha zinazotumika ni kodi ya watanzania.
Hata hivyo aliainisha viwanja vingine vinavyofanyiwa ukarabati ni uwanja wa Kigoma, Musoma, Bukoba, Shinyanga huku akisisitiza sekta ya ujenzi na uchukuzi inaendelea kuimarika kwa kasi.
Mayongela TAA inakabiliwa na changamoto ya gari la zimamoto kitendo kinachosababisha baadhi ya viwanja kutokuwa na huduma ya ndege ambapo aliongeza kwamba mpaka sasa wana gari 10 mpya ambazo zilinunuliwa katika bajeti ya 2016/2017, 2017/2018.
Pia alisema TAA imekusudia kujenga kiwanja cha ndege katika Mkoa wa Simiyu ambacho kitakuwa karibu na Hifadhi ya Taifa ya Mbunga ya Serengeti kitakachosaidia watalii wa ndani na nje kufika hapo.
Naye Waziri Kamwelwe alitoa wiki moja uwanja ndege wa Mwanza kufanyiwa marekebisho madogo madogo kabla ya Julai 29, mwaka huu ili ndege kubwa ya dreanline iweze kutua salama.Hata hivyo alisisitiza kuendelea na uboreshaji wa jengo la abiria, zimamoto na kifaa cha hali ya hewa.
Katika hatua nyingine, Kamwelwe alisema Julai 29, mwaka huu atakuwa Mwanza kwa ajili ya kuingia mkataba wa ujenzi wa ukuta kuzungushia uwanja wa ndege pamoja na uzinduzi wa Kivuko cha MV Mwanza ambacho kitafanya safari zake kati ya Busisi-Kigongo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.