WAFANYABIASHARA KANDA YA ZIWA KUNUFAIKA NA SILENT OCEAN
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda kwa ushirikiano na Kampuni ya usafirishaji kwa njia ya maji Silent Ocean wameazimia kwa pamoja kukutana na Wafanyabiashara wa Kanda ya Ziwa na kuhakikisha kila mmoja ananufaika na usafirishaji wa mizigo kutoka Nchi mbalimbali duniani.
Maazimio hayo yamefanyika leo Februari mosi Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa alipotembelewa na Balozi Ndugu Mwemba Burton na wawakilishi wa kampuni hiyo waliowasili Mkoani humo kwa ajili ya Kampeni ya Mtaa kwa Mtaa ikilenga kuitangaza kampuni ya Silent Ocean Mkoani Mwanza.
Akizungumza mara baada ya kuwakaribisha Mhe. Mtanda amesema Wafanyabiashara wa Mwanza watawapa ushirikiano wa kutosha na amewataka pia Wafanyabiashara hao kutumia Kampuni hiyo ili kuepukana na usumbufu wa kupoteza mizigo mara kwa mara.
Sambamba na hilo pia RC Mtanfa ameweka wazi jinsi miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itakavyoboresha huduma ya usafirishaji wa mizigo kupitia njia ya anga, ardhi pamoja na maji (Ziwa Viktoria) na kuongeza mapato ya Mkoa.
“… zaidi ya bilioni 30 zimetengwa kwa ajili ya kutanua uwanja wa ndege, kuna Reli ya SGR, kuna ujenzi wa meli kubwa ya MV. Mwanza Hapa Kazi Tu yenye thamani ya bilioni Tsh.123 ambayo meli hiyo itaenda Kenya na Uganda kupitia Ziwa Viktoria, Uwekezaji huu mkubwa ukikamilika itarahisisha usafirishaji wa mizigo na abiria kwa kiasi kikubwa”.
Aidha RC Mtanda ameendelea kwa kusema Serikali inatambua umuhimu wa sekta binafsi, na kwa kuwa imeajiri watu wengi wakiwemo wafanyakazi wa Silent Ocean hivyo amesema ili wafanye shughuli zao vizuri lazima wewekewe mazingira wezeshi huku Serikali ikitegemea pia kupata kodi.
Kwa upande wa Balozi wa Silent Ocean Mwemba Burton amempongeza na kumshukuru Mkuu wa Mkoa kwa mapokezi mazuri, huku akihusianisha maono ya Viongozi wa serikali na Silent Ocean yanavyoendana na kueleza jinsi Kampuni hiyo inavyofanya kazi na kuhakikisha mizigo inafika kwa wakati na kwa Usalama wa hali ya juu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.