Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amewataka wafanyabiashara ndogondogo mkoani humo kuwa na nidhamu ya shughuli zao ili kuendeleza mitaji na kupata faida zenye tija.
Ametoa wito huo leo Septemba 02, 2025 wakati akihutubia katika kongamano la wafanyabiashara ndogo ndogo wa Mkoa huo lililowakutanisha makundi mbalimbali wakiewemo Machinga, Maafisa Usafirishaji (Bodaboda & Bajaji), Wasusi, Washonaji, Mama Lishe, Baba Lishe na waendesha Guta.
Mhe. Mtanda amesema biashara inahitaji kujielimisha hususani masuala ya mitandao ili kujua ni taasisi gani inatoa hifadhi ya jamii na waweze kujiunga pamoja na kujihakikishia ulinzi wa mitaji kwa kujisajili kwenye bima kama za moto na ajali.
Aidha, amewapongeza wajumbe wa kongamano hilo kwa kupata elimu ya masuala mbalimbali hususani kuzifahamu taasisi za kifedha zinazokopesha mitaji na akatoa wito kuzingatia elimu iliyotolewa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bima nchini (TIRA) ili kulinda biashara zao.
“Mtembea bure sio sawa na mkaa bure, mmejifunza mengi na nawapongeza waandaaji wa kongamano hili kwa kugusa kila rika na kundi kuhakikisha wanawajengea uwezo katika masuala mbalimbali, nendeni mkayafanyie kazi na kuwafikishia wengine elimu mliyopata.” RC Mtanda.
Vilevile, ametumia wasaa huo kuwaalika kushiriki Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 kwa kuanza kushiriki kwenye kampeni na uchaguzi wenyewe kwa amani na utulivu.
Akisoma risala ya wafanyabiashara ndogondogo Ndugu Aziz Jabir ametumia jukwaa hilo kutoa shukrani kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwajengea ofisi katika Mikoa yote na kuwaletea vitambulisho vinavyowafanya watambulike na kupewa mikopo na taasisi za kifedha kote nchini.
Aidha, ameipongeza serikali kwa kuchochea shughuli zao kwa uboreshaji wa miundombinu ya barabara, Maji, Bandari, Reli na Vivuko nchini na akabainisha changamoto ya usajiri unaolegalega kwani ni wafanyabiashara elfu 2 pekee kati ya zaidi ya elfu 6 waliopo Mwanza ndio wamesajiriwa na kukwamisha ukopaji wa fedha za mitaji.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.