Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda ametoa wito kwa wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya afya kwa kuchangia nguvu kazi hususani katika hatua za awali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Mhe. Mtanda ametoa wito huo alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Manayi Wilaya ya Kwimba wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa Zahanati ya Manayi inayojengwa katika Kijiji cha Igaga. Ameeleza kusikitishwa na kusuasua kwa baadhi ya wananchi kuchangia nguvu kazi katika ujenzi wa zahanati hiyo.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kuwekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu na huduma za afya kwa ujumla hivyo ni muhimu wananchi kuwa sehemu ya maendeleo hayo kwa kushiriki kikamilifu kupitia shughuli kama kusomba mawe, mchanga na kufyatua matofali.

Ili kuhimiza uwajibikaji Mhe. Mtanda ameonya kuwa Serikali inaweza kuhamishia fedha za ukamilishaji wa zahanati hiyo kwenda eneo jingine endapo ndani ya mwezi mmoja wananchi hawataonesha juhudi na nia ya dhati ya kuchangia ujenzi wa miundombinu hiyo.

“Tumewasikia wananchi wa Kijiji cha Manayi kupitia kwa Mkuu wa Wilaya wakieleza kuwa jitihada zao zimekwama licha ya Serikali kutoa fedha za ukamilishaji. Baada ya mwezi mmoja, wasije wakalaumu maamuzi yatakayochukuliwa,” amesisitiza Mkuu wa Mkoa.

Akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi Mtendaji wa Kata ya Ilula, Bi. Hope Longino amesema kuwa mwezi Julai 2025 Serikali ilitoa shilingi milioni 300 kwa ajili ya ukamilishaji wa maboma matano ya zahanati zilizopo katika vijiji vya Igaga, Shirima, Kawekamo, Bugunga na Kijida.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.