*Wilaya ya Magu yavuka lengo kwa Ujenzi wa vyumba vya Madarasa*
Bilioni 3.26 zajenga Madarasa 163 wilayani Magu kwa ajili ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza 2023 na kupelekea wilaya hiyo kuwa na ziada ya vyumba saba vya Madarasa ambavyo vitatumiwa na vidato vingine kutokana na mahitaji kuwa ni vyumba 271 kutokana na uwepo wa vyumba 115 hivyo kupelekea kuwa na vyumba 278.
Hayo yamebainishwa leo (Januari 04, 2023) wakati wa hafla ya uzinduzi iliyofanyika kwenye shule ya Sekondari Magu iliyojengewa vyumba 12 vya madarasa kati ya shule 28 zilizopata mradi huo ambapo kwa wilaya nzima jumla ya wanafunzi
10823 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu.
Akizungumza na wananchi kwenye uzinduzi wa Madarasa hayo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Adam Malima ametoa pongezi kwa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa upendo wake kwa wanafunzi kwa kuamua kuwaboreshea mazingira ya Elimu.
"Kwa mikoa yote nchini sisi Mwanza ndio tumeongoza kwa kupewa Madarasa 983 kupitia mradi huu, nawasihi wananchi tusiache kumuombea dua Rais wetu mpendwa kwa Mwenyezi Mungu ili amjaalie afya njema aendelee kuwahudumia wananchi wake." Malima.
Amesema, Serikali inatarajia ongezeko kubwa la wanafunzi kutokana na jamii kuzidi kuzaliana na kwamba imejipanga kuendelea kuboresha Miundombinu si tu ya wanafunzi bali na walimu na ametoa rai kwa wanafunzi kutunza madarasa na samani na kusoma kwa bidii ili ufaulu upande.
"Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwani kila shule wilayani kwetu imefikiwa na mradi huu kwa kupata idadi tofauti ya vyumba vya Madarasa lakini tumepata pia shule mbili mpya kabisa na ilipofika tarehe 24, Disemba 2022 tulikua tumeshakamilisha ujenzi wa madarasa haya." Amesema Mkuu wa wilaya ya Magu, Mhe. Salum Kalli.
Afisa Elimu Sekondari wa wilaya hiyo Bi. Beatrice Balige amesema pamoja na ukamilishaji wa madarasa hayo jumla ya seti za viti na meza 6520 vipya vimetengenezwa na kufikia lengo la uboreshaji wa Elimu kwa kuwafanya watoto waketi kwenye Madarasa yanayochagiza ufundishaji na kujifunza kwa ufanisi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.