*Wizara ya Afya yaanza kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Bima ya afya kwa wote.
Wizara ya Afya imeanza kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa Bima ya Afya kwa wote wakati muswada huo ukiwa mbioni kupitishwa na Bunge lijalo.
Akizungumza na wawakilishi wa makundi mbalimbali ya Jamii kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amesema takwimu zinaonesha ni asilimia 15 tu Watanzania wapo katika mfumo wa bima ya sasa na asilimia 85 wapo nje ya utaratibu huo ambayo ni idadi kubwa inayopata usumbufu wa huduma ya afya.
"Serikali ya awamu ya Sita imeangalia mbali na sasa kuja na huo mpango wenye ukombozi kwa kila Mtanzania ambaye atakuwa na uhakika na matibabu bora,tukawe mabalozi wazuri katika kuwaelimisha wenzetu"amesisitiza Mtendaji huyo Mkuu wa Wizara.
Prof.Makubi amebainisha muda huu wa miezi sita utumike kikamilifu kuelimishana ili muswada huo utakapopitishwa na Rais Dktr Samia Rais na kuanza kufanya kazi Julai Mosi mwaka huu uwe na tija kwa Wananchi na Serikali ambayo itazidi kutoa huduma bora kwenye Sekta hiyo.
"Sisi tunazidi kumuombea Rais wetu ambaye ameonesha dhamira ya vitendo ya kumpigania kimaendeleo mwananchi wake,tunaahidi kuwa waelimishaji wazuri kwa wenzetu" Mchungaji Jacob Mutash
"Kundi letu lipo katika mazingira hatarishi sana tunapata ajali kila kukicha tunaamimi sasa tumeangaliwa kwa jicho la tatu na Serikali yetu katika mpango huu mpya wa bima ya afya kwa wote "Katibu wa Chama cha boda boda Mwanza Makoye.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kutoka Wizara ya afya Rahibu Mashambo amesema baadhi ya maoni yaliyotolewa na wadau watayafanyia kazi kwani bado nafasi ipo ya kuufanyia maboresho kabla ya kuanza rasmi mpango huo.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau wa Sekta ya Afya na Taasisi zake,Marafiki wa Maendeleo katika huduma za afya,Viongozi wa Dini,makundi ya wawakilishi ya wavuvi,wakulima,Wafanyabiashara ndogo ndogo na bodaboda.
Tangu Tanzania ipate Uhuru mwaka 1961 Serikali ilibeba jukumu la kuwahudumia bure Wananchi wake na kuanzia miaka ya 90 ilibadili utaratibu huo kutokana na Serikali kuelemewa na mzigo huo na kutambulisha mfumo wa Wananchi kuchangia huduma ya afya.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.