ZAIDI YA BILIONI 2 KUNUFAISHA WANANCHI UJENZI WA MINARA YA MAWASILIANO MWANZA
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye (MB) amesema Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa minara 758 unaogharimu zaidi ya Bilioni 200 utakaonufaisha wananchi Milioni 23.6 kupata huduma bora za mawasiliano ya intaneti, data na simu.
Mhe. Nape amebainisha hayo leo Julai 18, 2024 Wilayani Sengerema alipokua ziarani kukagua mnara wa mawasiliano katika Kisiwa cha Lyakanyasi huku akibainisha kuwa wilaya hiyo itanufaika kwa kujengewa minara 2 kati ya 17 inayojengwa Mwanza.
"Minara hii inajengwa na makampuni ya simu tena inagharimu fedha nyingi sana zaidi ya Milioni 350 kwa mnara mmoja tena kwenye maeneo ambayo hayana mvuto sana kibiashara na kwakweli makampuni mengine yasingeweza kwenda kuwekeza hivyo ni lazima ilindwe." Mhe. Nnauye.
Vilevile, amewasihi viongozi wa wilaya kusimamia upatikanaji wa maeneo ya kujenga minara hiyo itakayosaidia kukuza uchumi vijijini na akatoa wito kwa taasisi zinazotoa huduma za umeme na barabara kufikisha miundombinu hiyo kwa kipaumbele ili kurahisisha utoaji wa huduma bora pamoja usalama.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutenga zaidi ya Tshs. Bilioni 2.4 kwa ajili ya kujenga minara 17 katika kata 16, vijiji 52 na inatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi 296, 410 wa wilaya 5 za Magu, Ilemela, Sengerema, Misungwi na Ukerewe.
Akiwasilisha taarifa ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA) John Dafa amesema hali ya mawasiliano nchini ni ya kuridhisha kwa zaidi ya asilimia 85 (2G, 3G, 4G) na kwa Mwanza huduma zimefika kwa wananchi kwa wastani wa zaidi ya asilimia 95.
Akizungumzia usajili wa laini za simu amesema Mwanza kuna ongezeko la zaidi ya asilimia 42 kutoka mwaka 2022 kwani wananchi 4,803,249 (Machi 2024) wamesajiliwa kutumia laini za simu na kwamba kuna zaidi ya vituo vya redio 26 mkoani humo kwa sasa.
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF) Bi. Justina Mashiba amesema hakuna mtanzania atakaa bila huduma za mawasiliano na kwamba siku za nyuma minara 50 ilijengwa kupitia ruzuku ya awali UCSAF kwa zaidi ya Bilioni 6.6 huku wananchi 885, 420 wakinufaika mkoani Mwanza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.