Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni nchini (BRELA) imetambulisha mfumo mpya wa kutuma maombi ya leseni ya biashara kwa wadau wa biashara utakaokuwa unafanyika kwa njia ya mtandao badala ya kutumia fomu za kawaida ili kuwasaidia kupata kibali kwa wakati.
Akizungumuza jijini Mwanza wakati wa semina elekezi kwa wadau wa biashara, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha kutoka Brela, Bakari Mketo alisema mfumo huo unakuja kutatua changamoto ya mlolongo mrefu wa uombaji leseni za biashara ambapo hivi sasa leseni itatolewa punde tu baada ya taarifa zitakapohakikiwa na malipo kufanyika.
“Tupo hapa kuleta elimu ya utoaji wa leseni kwa njia ya mtandao, kama mnavyojua tulitangulia kufanya hivyo kwa upande wa makampuni, majina ya biashara, alama za biashara na leseni za viwanda na sasa Brela tumepewa jukumu jipya la utoaji wa leseni daraja la kwanza ‘Class-A’ ambayo awali ilikuwa inatolewa na wizara ya viwanda na biashara.
“Na kwa sababu hii leseni hii ina uhusiano mkubwa na leseni daraja la pili ya class-B zinazotolewa na halmashauri, hivyo ili kuepusha kutoa leseni tofauti kwenye nchi moja kwa wadau wetu lazima leseni hizi zitoke zikiwa zina sura moja na namna moja ya upatikanaji, hivyo zote kwa pamoja zitapatikana kwa njia ya mtandao ili kumpunguzia milolongo mirefu mteja wetu kwa maana ya gharama na muda.
“Sasa tupo kwenye hatua za awali za upandikizaji mfumo huu kwenye halmashauri sita zilizochaguliwa ambazo ni Mwanza, Bukoba, Karagwe, Ilala, Chalinze na Mafinga kabla ya kurasimishwa nchi nzima kwani halmashauri hizi zitatoa picha kamili ya mwenendo wa mfumo huu ili kama kuna changamoto tuzifanyie kazi mapema,” alisema Mketo.
Kwa upande wake Makamu wa Rais wa Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Joseph Kahungwa alisema kuwa mfumo ulioanzishwa na Brela ni mzuri pia ni kama neema kwa wajasiliamali wapya kwani utawapunguzia wafanyabiashara usumbufu wa kufunga safari kwenda makao makuu Dar es Salaam kufuata leseni ya biashara.
“Mimi kama mdau wa biashara nimependa mfumo huu ingawa tumewaomba wahusika kurahisisha zaidi hasa kwa kutengeneza mfumo ambao vibali vyote vitatolewa kwenye nyaraka moja itakayoambatanishwa badala ya kuwa na nakala tofauti tofauti za vibali ili kurahisisha zaidi zoezi la kutuma maombi,”alisema Kahungwa.
Naye Afisa Biashara kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Josephine Lyimo amesema mbali ya mfumo huo kuokoa muda wa upatikanaji leseni za biashara pia utasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza mianya ya rushwa waliyokuwa wakikutana nayo wafanyabiashara wakati wa ufuatiliaji wa leseni zao, hivyo itachagiza wajasiriamali wengi wapya kufanikisha adhima yao.
Semina hiyo iliyofanyika kwa muda wa siku tano mfululizo imewakutanisha kwa pamoja wafanyabiashara, wanasheria, wakaguzi wa mahesabu, TCCIA, pamoja na Brela wenyewe ili kuongeza uelewa zaidi wa mfumo huo mpya kwa wadau tofauti wa biashara na kuondoa ugeni wa mfumo huu kwa watanzania wote kwa ujumla.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.