Wito umetolewa kwa watu wenye tatizo la shinikizo la damu kufanya mazoezi na kuepuka ulaji usiopangiliwa huku tahadahari ikitolewa kwa wanaojikita kutumia tiba asili ambazo hazijafanyiwa utafiti.
Wito huo umetolewa na Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya figo na shinikizo la damu wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando Ladislaus Rudovick,wakati hospitali hiyo ikiadhimisha siku ya Shinikizo la Damu Duniani kwa kutoa huduma za upimaji afya bure kwa magonjwa yasiyoambukiza.
Dkt.Rudovick alisema,suluhisho la kwanza kwa mtu mwenye tatizo la shinikizo la damu ni kufanya mazoezi na kuepuka ulaji usiopangiliwa.
Huku akitoa tahadhari kwa wale wanaojikita zaidi kwenye tiba asili ambazo hazijafanyiwa utafiti kwani moja ya changamoto ni kupata madhara mengine yanayoweza kusababisha matatizo zaidi ya kiafya, ikiwemo kuharibu figo.
Akizungumzia ugonjwa wa shinikizo la damu Dkt.Rudovick, alisema ugonjwa huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili ambapo ya msingi hubainika zaidi kwa wale wenye umri wa kati ya miaka 30 hadi 50 na chanzo chake kwa asilimia 90 hadi 95 huwa hakijulikani.
Huku ya sekondari ni chini ya umri wa miaka 30 au zaidi ya miaka 55 ambayo chanzo chake hujulikana na wakiondoa chanzo basi tatizo linakwisha jumla.
Alisema,baadhi ya visababishi ni pamoja na mishipa ya kwenye figo kuwa miembamba, uvimbe tumboni na matatizo ya tezi yanayopelea homoni mwilini kuongezeka pamoja na mfumo wa maisha ambao unaweza kuwa chanzo kikubwa hasa kwa watu wenye kipato kizuri kinachopelekea ulaji usiopangiliwa pamoja na kukosa muda wa kufanya aina yoyote ya mazoezi.
“Utakuta mtu anatoka ndani kwake na kuingia kwenye gari hadi ofisini huku muda wa kazi ukiisha anaingia tena kwenye gari, anapita sehemu za burudani, anaagiza nyama, tena ile nyekundu na kileo, hasa bia, kisha anarudi nyumbani anaoga na kulala, na kesho yake hivyo hivyo,”alisema.
Kwa upande wake Daktari Nelly Mwageni,alisema magonjwa ya ngozi nayo pia huendana na umri wa mtu ambapo watoto chini ya umri wa miaka 12 wao husumbuliwa zaidi na pumu ya ngozi ambayo chanzo chake mara nyingi ni kurithi kutoka katika ukoo na baadhi ya dalili ni kuwashwa macho na mafua ya mara kwa mara.
“Mara nyingi hujitokeza kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa,mwingine mvua nyingi au joto kali ni tatizo na mwingine msimu wa mazao kutoa maua ni shida,mfano ule ungaunga unaotoa maua ya mahindi ukimpata mtoto wa tatizo hilo anaathirika,” alisema.
Ambapo vijana mara nyingi hupatwa na tatizo la mba na chunusi kutokana na balehe, wazee ni ngozi kuwa kavu kutokana na upungufu wa uwezo wa mwili kuzalisha mafuta.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.