Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella amekabidhi pikipiki 18 zenye thamani ya takribani Tshs.54,000,000/= zilizotolewa na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa ajili ya Maafisa Elimu Kata 18 waliomo ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza.
Akitoa hotuba wakati wa kukabidhi pikipiki hizo kwa niaba ya mkurugenzi wa Jiji la Mwanza Kiomoni K. Kibamba, Kaimu Mkurugenzi Philipo Kajura Mukama amesema, ili kuimarisha usimamizi na matumizi sahihi ya pikipiki hizi Maafisa Elimu Kata wanapaswa kuzingatia taratibu walizopewa.
"Mtumiaji wa pikipiki awe na leseni inayomruhusu kutumia chombo cha moto,itumike ndani ya Kata husika tu na itumiwe na Afisa Elimu Kata na si mtu mwingine,itumike muda na siku za kazi pia zisitumike kubeba mizigo na abiria,"alisema Mukama.
Naye Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza Mhe. James Bwire amesisiza kwa wadau wote wa Jijini hapa kuhakikisha wanaiunga mkono Serikali katika juhudi za Maendeleo kwani inafanya kazi kubwa kuhakikisha Elimu inakwenda mbele.
"Vifaa hivi vimetolewa kwa madhumuni maalumu ya kuhakikisha Elimu inasonga mbele hivyo pikipiki hizi zitumike kwa madhumuni hayo na si vinginevyo, itawaghalimu mkitumia kwa matumizi binafsi,"alisema Bwire.
Hata hivyo,Mhe.Mongella amesisitiza kuwa Serikali ya awamu ya tano imejikita kuimarisha Sekta ya Elimu hivyo kila mwalimu ana wajibu wa msingi wa kuiwezesha Sekta hii izidi kusonga mbele kwa kila mwalimu kutimiza wajibu wake.
"Halmashauri zote 8 za Mkoa zimepata pikipiki hizi za Maafisa Elimu Kata,walimu Mwanza mnafanya kazi nzuri,changamoto zipo kikubwa tuendelee kuahirikiana na Serikali na mifumo yake yote ili kutatua changamoto hizi,"alisema Mongella.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.