Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (MB) amewaahidi wananachi wa Mkoa wa Mwanza kuwa serikali imeishatenga fedha za kukamilisha miradi yote ya kimkakati na maendeleo inayotekezwa ndani ya Mkoa huo.

Dkt. Nchemba amesema hayo leo Disemba 6, 2025 wakati akizungumza na wanachi wa Mkoa wa Mwanza katika kiwanja cha Nyamagana mara baada ya kukagua maeneo mbali mbali ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku moja mkoani humo.

Aidha, amewataka viongozi wa mikoa kuhakikisha wanazisimamia hospitali katika kutoa huduma za dharula kwa wagonjwa bila kusubilishwa kisha utaratibu wa uandikishaji utafata baadae.

“Kwa yeyote atakaefika hospitali kwa dharula aanze kwanza kupatiwa huduma alafu uandikishaji utafata baadae, hospitali shughulikieni mambo ya dharula msisubirishe wajawazito”. Amesema Mhe. Dkt. Nchemba.

Sambamba na hayo, Dkt. Nchemba amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda kwa kuweka utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi kila siku za jumanne huku akimtaka aweze kuwatembelea wananchi katika maeneo yao ili aweze kutatua kero zao mbalimbali.

Akimkaribisha Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda amesema uongozi wa mkoa umejipanga kuhakikisha wanaimarisha usalama wa mkoa lakini pia usalama wa wananchi na mali zao kwa ujumla.

Mhe. Mtanda ameongeza kwa kuiomba serikali kuweza kukamilisha miradi ya kimkakati na kimaendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo ikiwemo mradi wa treni ya kisasa ya umeme SGR ambayo mpaka sasa imefika asilimia 64 ili izidi kuufungua mkoa kiuchumi.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.