Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi kwenye ujenzi unaoendelea wa jengo la abiria la uwanja wa ndege Mkoani Mwanza litakalogharimu zaidi ya bilioni 13.2.
Akizungumza wakati wa uwekaji jiwe hilo Mhe.Majaliwa alisema,Serikali ya awamu ya tano imedhamiria kutekeleza miradi mikubwa inayogusa maisha ya wananchi ya kila siku ikiwemo la ujenzi huo.
Majaliwa alisema, viongozi wa Mkoa wanapaswa kuusimamia mradi huu vizuri na ukamilike kwa muda kwani ni kichocheo cha uchumi na Maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Aidha aliwataka wataalam pamoja na wafanyakazi wote waliopata nafasi ya kuajiriwa katika mradi huo kufanya kazi na kuhakikisha unakamilika kwa wakati ili uweze kuwanufaisha watanzania kama livyokusudiwa.
"Mradi huu utaleta manufaa makubwa sana, kwa hiyo naweka jiwe la msingi baada ya kuambiwa kwamba hatua ya ujenzi wa msingi imefikia asimilia 90 na nina uhakika kufikia mwezi wa tatu mpaka mwezi wa nne litakuwa limekamilika.
Aidha mmeeleza kuwa chanzo cha fedha mlizopata zinatokana na mapato ya ndani yaliyotolewa na Halmashauri hizi mbili hivyo sehemu ya fedha iliyobaki Serikali itaweka mchango wake," alisema Mhe.Majaliwa.
Kwa upande wake Msimamizi Mkuu wa Mradi huo Mhandisi Tunaye Mahenge alisema, utekelezaji wa ujenzi wa jengo kuu ulianza rasmi Septemba 19 mwaka huu na unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 30, 2020 huku ukigharimu Bilioni 13,260,271,951.
"Kwa sasa hivi chanzo pekee cha fedha za utekelezaji wa mradi huu ni shilingi Bilioni 4 ambazo zinatokana na makusanyo ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambayo imetoa shilingi Bilioni 2.2 huku Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela ikichangia shilingi Bilioni 1.8,"alisema Mhandisi Mahenge.
Aliongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo unatekelezwakwa kuwatumia wataalam wa ndani wa Serikali kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na mafundi (Force Account) ikiwemo ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Halmashauri za Jiji la Mwanza na Manispaa ya Ilemela, Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Mamlaka ya Uwanja wa Ndege Mwanza.
Pia alisema,jengo hilo litakuwa na ukubwa wa takribani meta za mraba 40,000 uwezo wa kuhudumia zaidi ya abiria laki nne (400,000) kwa mwaka,ukumbi mkubwa wa abiria wa ndani wenye uwezo wa kuhudumia abiria 400 kwa wakati mmoja,ukumbi wa abiria wa kimataifa wenye uwezo wa kuhudumia abiria 200 kwa wakati mmoja.
Sanjari na kumbi za abiria mashuhuru kama vile viongozi zenye uwezo wa kuhudumia abiria 140 kwa wakati mmoja,migahawa, maduka na maeneo ya kuhifadhia mizigo,ofisi mbalimbali zikiwemo za TRA,uhamihaji,afya,polisi, Maliasili na watumishi tofauti tofauti,eneo la maegesho ambalo litakuwa na uwezo wa kuhudumia takribani magari 320 kwa wakati mmoja pia wakati wa utekelezaji wa mradi huu hususani hatua ya msingi wafanyakazi 150 hadi 200 kila siku wamaekuwa wakitumiwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela alisema,ofisi ya Mkoa ilichukua jukumu la kusimamia utekelezaji wa mradi huu ikiwa ni pamoja na kuunda kamati ya ujenzi,kusanifu michoro ya jengo, kusimamia makusanyo na matumizi ya fedha pamoja ujenzi kwa ujumla wake.
Mhe.Mongela alisema,wanatarajiia mradi huu utachochea kwa kiasi kikubwa ukuaji wa sekta ya utalii eneo la Kanda ya Ziwa na taifa kwa ujumla kwa kuwa ni jiji linalozungukwa na vivutio vingi vya utalii kama vile mbuga za wanyama, Ziwa Victoria na vivutio vya kitamaduni.
Hata hivyo alisema,kukamilika kwa utekelezaji wa mradi huu kutaimarisha ulinzi na usalama katika jiji hilo ikiwa ni pamoja na Kudhibiti utoroshwaji wa maliasili kama vile madini,nyara za Serikali,uingizaji na usafirishaji wa madawa ya kulevya na kemikali nyingine haramu pamoja na wahamiaji haramu.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.