Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe John Mongella amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza,kuhakikisha jengo jipya la wagonjwa wa nje(OPD)la hospitali ya halmashauri hiyo linakamilika kabla ya Juni 30, mwaka huu.
Mhe.Mongella alitoa agizo hilo mara baada ya kutembelea hospitali hiyo wakati wa ziara yake ya kukagua shuguli za maendeleo Wilayani Magu ikiwemo hospitali hiyo, mradi wa maji Magu mjini,REA Bugabu na Bonde la Kandawe kwa ajili ya kuangalia shughuli za kilimo cha mpunga, alisema hawawezi kuwa na kitu kimoja tu hivyo wamalizie jengo hilo ili waanzishe suala jingine.
Mhe.Mongella alisema, Mkurugenzi anapaswa kuhakikisha anakamilisha jengo hilo kabla ya kuanza kwa mwaka mpya wa fedha wa kiserikali ili liweze kutoa huduma kwa wananchi.
"Jitahidi kabla ya kuanza mwaka mpya wa fedha uwe umekamilisha jengo hili,ambapo tutamualika Waziri Mkuu au Rais akiwa anapita atuzindulie jengo letu na wananchi waanze kupata huduma kupitia katika jengo hilo," alisema Mongella.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Magu George Lutengano, alisema ofisi ya Rais TAMISEMI iliwaletea fedha milioni 200,kwa ajili ya kufanya ukarabati wa jengo la wagonjwa wa nje la zamani,lakini ni chakavu na wakafikiri siyo busara kuweka fedha hizo katika jengo hilo ambalo ata ukarabati wake usinge onekana vizuri.
Hivyo waliona fedha hizo kujenga jengo jipya kwa ajili ya wagonjwa wa nje ambapo waliwasiliana na Wizara wakawahaidi kuwa watawaongezea fedha ili kukamilisha ujenzi huo,lakini wakiwa wanasubilia fedha hizo hawawezi kukaa hivyo watakata fedha za mapato ya ndani ya halmashauri na zinazokusanywa kutoka hospitali ili kuendelea kufanya kile kinachowezekana.
"Mkuu wa Mkoa ametushauri kuwa vyovyote tutakavyo fanya tujitahidi ili jengo kabla ya mwaka huu wa fedha kuisha basi liwe limeisha na kuweza kutoa huduma kwa watumishi na wananchi kwani jengo tulilonalo kwa sasa hali yake siyo nzuri,kimsingi tulivyopata milioni 200 wengine walituambia kuwa hatuwezi kujenga hili jengo kama mnavyoliona,mimi sipendi kukata tamaa tutakaa na wenzangu tutafanya linalowezekana tunaona tunatekeleza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa ili liweze kutoa huduma kwa maslahili ya wananchi wetu ambao wanahangaika,tutapigana na tutafika tunapo fika ili watu waanze kupatiwa huduma hapa ifikapo Julai," alisema Lutengano.
Hata hivyo alisema,jengo hilo litaweza kuwahudumia wagonjwa wote wa rufaa wanaoletwa kwa ngazi ya Wilaya kwa sababu kuna vyumba vya madaktari vya kuona wagonjwa siyo chini ya 8,chumba kidogo cha upasuaji,vyumba vya wauguzi na dawa,ni la kisasa ambalo limezingatia ramani mpya iliyotolewa na ofisi ya Rais TAMISEMI,hivyo wanaamini lutakidhi mahitaji ya wananchi wa Magu litakapo kamilika ambapo ujenzi umechukua miezi mitano na hiyo ni kutokana na uhaba wa fedha.
Nao baadhi ya wananchi wa Wilayani Magu, walisema endapo jengo hilo litakamilika litawasaidi kupunguza msongamano na kupata huduma kwa haraka,hivyo walimshukuru Mhe. Rais kwa juhudi zake za kuwasaidia wananchi na kuboresha sekta ya afya ikiwemo ujenzi wa vituo vya afya na dawa.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.