Mwanza Yajipanga kutokomeza ongezeko la watoto wa Mitaani
Wizara ya Afya kupitia idara kuu ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Mwanza wameweka mikatati ya pamoja ya kuunganisha watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani ili kurudi katika familia zao.
Akizungumzia ongezeko la watoto wa Mitaani Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella amesema kupitia tafiti zilizofanywa na Head Count lililoendeshwa na wadau wa Railway Children Africa na Cheka sana Tanzania 2017 umetambua jumla ya watoto 1254 walio katika mitaa yetu, 978 walitambuliwa wakati wa mchana na usiku ni watoto 276 kuwa wanalala na kufanya shughuli mbalimbali za mitaani wakati wa usiku.
"Kuna haja ya kutambua hawa watoto kwa kupitia viongozi wa vijiji, mitaa na vitongoji na mimi naunga mkono sana Mwanza tuko tayari kama ni kuanza kulikabili, tupo tayari kushirikiana na Wizara,wadau wote na si kwa maana ya kuwanyanyasa bali kuwajenga wawe raia wema kwenye jamii hata kwenye Taifa.
Aidha ameyataadharisha mashirika na wadau wanaotoa misaada kwa watoto wa mitaani ambayo huwasaidia wiki nzima na kukiri kuwa inaongeza ongezeko la watoto wa mitaani kwani wanapata mahitaji, hivyo amewaomba wadau waungane ili kuwarudisha majumbani.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto Dkt. John Jingu amesema zipo sababu nyingi zinazosababisha tatizo la watoto kuja mitaani ambazo ni pamoja na vifo vya wazazi au walezi wa watoto,ugomvi wa wazazi na malezi potofu yasiyojali haki za watoto, ukatili pamoja na umaskini kutoka kwenye familia.
"Sheria imeeleza majukumu ya makundi mbalimbali katika kumlea mtoto ambapo kati ya makundi haya ni familia,jamii na mamlaka za Serikali za Mitaa,hivyo wafundishwe malezi sahii ya kustawisha jamii zetu,"alisema Dkt.Jingu.
"Kuweka kumbukumbu za watoto waishio katika mazingira hatarishi, pia kufanya ufuatiliaji wa watoto hao, wafanyiwe uchunguzi pia tukubaliane warudishwe majumbani kwao kwani sheria ya mtoto ya mwaka 2009 inaruhusu," alisema Dkt.Jingu.
Kwa upande wake Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt.Naftali Ng'ondi awali akiwakaribisha wadau katika kikao amesema Wizara yetu ya Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto kwa muda mrefu imekuwa na mazungumzo na Mkoa wa Mwanzajuu ya kuwa na mpango kabambe na endelevu wa kushughulikia tatizo la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi.
" Mpaka sasa kwa mujibu wa Taarifa ambazo tunazo una jumla ya watoto 1254 ambao wanaishi na kufanya kazi mitaani,tunafahamu kwamba takribani asilimia 90 tunawafahamu wazazi wao, hivyo tumekutana hapa kuja kujadili na kuja na mpango ambao utatuwezesha kulishughulikia tatizo hili vizuri zaidi,"alisema Dkt.Ng'ondi.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.