Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. Said Mtanda leo tarehe 22 Desemba, 2025 amezindua rasmi ugawaji wa pikipiki kwa vijana wa Ilemela chini ya ufadhili wa Mhe. Mbunge wa jimbo hilo ikiwa ni utekelezaji wa ahadi aliyoitoa wakati wa kuomba ridhaa ya kuliongoza jimbo hilo.

Akizungumza na wananchi katika tamasha lililofanyika katika viwanja vya Furahisha Mhe. Mtanda amewataka vijana walionufaika na mkopo huo kuwa waadilifu na waaminufu na kuhakikisha wanadumisha amani ya nchi wakiwa katika shughuli zao za kujikwamua kiuchumi na sio kuvunja amani ambayo ni tunu ya taifa.

Amesema kuwa serikali mkoani Mwanza imedhamiria kuwainua vijana kiuchumi na kwamba imeanzisha kanzidata ya kuwatambua na kuweka mikakati ya kuwaendeleza katika stadi za maisha pale itakapobidi ili mwisho wa siku wawe na nyenzo, mtaji na vifaa vya kujitafutia.

Aidha, amempongeza Mhe. Mbunge kwa kutimiza ahadi kwa wananchi wa Ilemela kupitia mpango kazi aliojiwekea wa kuhakikisha anawapatia mitaji ya kujiimarisha kiuchumi hususani kundi kubwa la vijana ambalo ameanza nalo.

“Serikali ina mipango thabiti ya kuwainua vijana kiuchumi ikiwemo kuanzishwa kwa wizara maalumu ya kushughulikia vijana sio kwa sera pekee bali kwa kuwawezesha moja kwa moja vijana ili waweze kupiga hatua kiuchumi.” Mhe. Mtanda.

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe. Kafiti Kafiti amesema tamasha linalochagizwa na ugawaji pikipiki 100 ni katika kutimiza ahadi yake ya kuwakwamua kiuchumi walemavu, vijana na wanawake katika maeneo ya Mitaji ya kuweza kujiajiri.

“Utakuta Bodaboda anapewa pikipiki ya Milioni tatu na anatakiwa arejeshe milioni sita, gharama za leseni zimekuwa kubwa na ninaahidi kuwasemea ili ipungue kutoka elfu 70 hadi 30 na katika eneo la Mafunzo nataka kuwashika mkono kupitia VETA zetu.” Amefafanua.

Vilevile, amebainisha kuwa vijana hao kwa sasa watatoa Tshs. 10,000 pakee kupata mafunzo VETA badala ya 100,000 na amewawekea dhamana benki na kwamba kila baada ya miezi 6 atawapatia pikipiki 100 na kwamba watarejesha Tshs. 2,000 pekee kwa siku kama marejesho.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.