RC MAKALLA AWAPA KONGOLE NMB KWA KUWAUNGANISHA WATEJA KATIKA MFUMO RASMI WA KIFEDHA
*Asema kuwajumuisha watanzania kwenye mfumo rasmi wa kifedha kunasaidia kuinua kipato*
*Aipongeza kwa kubuni bidhaa zinazolenga mahitaji ya kila kundi kwenye soko na kwa kutoa mikopo*
*Atoa wito kuandaa programu kwa watumishi wengine wa serikali*
*Atoa wito kwa walimu kuhifadhi pesa benki na kuachana na mikopo yenye masharti magumu*
CPA Amos Makalla ameipongeza benki ya NMB kwa kuwatunza walimu kwa masuluhisho mbalimbali ya kifedha na kuunga mkono juhudi za Serikali za kuwajumuisha watanzania katika mfumo rasmi wa kifedha ili kuinua vipato vyao na uchumi kwa ujumla.
Ametoa pongezi hizo leo tarehe 15 septemba, 2023 kwenye warsha ya siku ya walimu iliyoandaliwa na benki hiyo ambayo imezindua mpango wa kuwafikia walimu zaidi ya 9,000 kote nchini kwa kaulimbiu ya "Mwalimu Spesho- Umetufunza Tunakutunza."
"Nimeambiwa kuwa madhumuni ya siku hii ni pamoja na kutambua mahusiano mazuri yaliyopo na kutoa fursa kwa walimu kutoa maoni na mapendekezo ya namna gani wanaweza kunufaika zaidi na huduma za benki hii, hakika jambo hili linatupa faraja sana kwakweli naomba niwapongeze sana NMB." Mhe. Mkuu wa Mkoa.
"Jitihada hizi ni nzuri na zinaunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya Sita katika kuhakikisha watanzania wanajumuishwa katika mfumo rasmi wa kifedha ili kuinua vipato vyao na uchumi kwa ujumla, natoa rai kwa mabenki na taasisi zingine za kifedha kuunga mkono ili elimu hii iwafikie wengi hasa maeneo ya vijijini." Amesisitiza Makalla.
Makalla amesema uamuzi wa kuwakutanisha walimu ni wa kizalendo na unafaa kuigwa na kila taasisi kwani unaonesha kuwajali walimu na utakuza mahusiano mazuri kati ya pande hizo mbili za benki na sekta ya elimu hapa nchini.
Vilevile, ametumia wasaa huo kuwapongeza kwa kubuni bidhaa zinazolenga mahitaji ya kila kundi kwenye soko na kwa kutoa mikopo mingi kwa wafanyakazi wa Serikali kuu na za mitaa ambapo asilimia kubwa ya walimu wananufaika nayo kwa kukidhi mahitaji ya familia na hata maandalizi ya maisha baada ya kustaafu.
"Nawasihi kuendelea kuandaa programu nyingi si kwa walimu tu hata kwa watumishi wengine wa Serikali ili kuwapa fursa ya kuongeza ufahamu wa huduma na muendelee kubuni huduma nafuu zaidi ambazo mfanyakazi wa kawaida anaweza kuzimudu." CPA. Makalla.
Aikansia Muro, Mkuu wa Idara ya wateja binafsi amesema kwa kipindi cha miaka 8 mfululizo wanakutana na walimu kwenye siku maalumu na makongamano hayo yamekua yakiwapa fursa kama wateja kuelimishwa juu ya huduma na inatoa nafasi kwa benki hiyo kupokea maoni juu ya huduma zao na kwenda kuziboresha.
"Benki ya NMB tutaendelea kuwa na masuluhisho bora ili kuwaleta watanzania pamoja na katika huduma bora za kifedha nchini, na tutaendelea kubuni huduma bora zaidi kwa ajili ya makundi yote nchini hata wafanyabiashara wadogo na wakulima." Bi. Aikansia.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.