*Trilioni moja zimetumika kuimarisha miundombinu ya usafiri wa majini Ziwa Victoria,Tanganyika na Nyasa: Mhe.Kihenzile*
Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe: David Kihenzile leo Novemba 17,2023 kwenye Bandari ya Mwanza South amefanya uzinduzi wa Meli ya MV Umoja na kusema Serikali ya awamu ya Sita imetumia jumla ya TShs. Trilioni moja kwa kufanya ukarabati wa Meli nyingine lengo likiwa kuimarisha uchumi kwa wakazi wa Kanda ya ziwana Taifa kwa ujumla.
Akizungumza na wakazi wa Mwanza waliofika kushuhudia hafla hiyo iliyokwenda pamoja na utiaji Saini wa ukarabati wa Meli za MV Ukerewe, Liemba na Nyangumi, Kihenzile amebainisha kuwa haijawahi kutokea kwa Serikali kutoa kiasi hicho kikubwa cha fedha hivyo wananchi wana kila sababu ya kumshukuru Rais Samia kwa vitendo kwa kufanya kazi kwa bidii.
"Mkoa wa Mwanza umekaa kimkakati hasa kutokana na kupakana na nchi za maziwa makuu hivyo kuimarika kwa miundombinu ya usafiri wa majini utaleta ongezeko kubwa la kibiashara na uchumi wa wananchi kuzidi kukua," Kihenzile
Ameongeza kuwa Meli ya MV Umoja ambayo itasafirisha mizigo kwa nchi za Uganda na Kenya ukarabati wake umeghatimu Shs bilioni 19, lengo la Serikali ni kuhakikisha kunakuwepo na tija katika shughuli za Uchumi kwa wafanyabiashara.
"Hii ni fursa ina kila sababu ya kuchangamkiwa na wananchi wetu kwani Meli hii ni kubwa na yenye uwezo wa kubeba shehena nyingi za mizigo,ni wakati wa kufanya biashara kubwa unaokwenda pamoja na muunganiko mzuri wa usafirishaji kuanzia Reli ya SGR", amesisitiza Mhe. Kihenzile wakati akizungumza na wananchi
"Huduma ya majini ni sekta muhimu kwa kanda ya ziwa na ukizingatia tumezungukwa na maji na ujio wa Meli hii utaleta matokeo makubwa ikiwa ni pamoja na kuchochea na kuchagiza maendeleo ya wananchi kwa sababu ya unafuu wa gharama za usafiri na uwezo wa kusafirisha shehena kubwa kwa wakati mmoja," Mhe. Amina Makilagi,Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana
Ameongeza kuwa kuwepo kwa MV Umoja utaendelea kuongeza wigo wa kibiashara uchumi wa nchi kukua, mapato ya meli kuongezeka hivyo na gawio la Serikali kuongezeka na kuwa kubwa, kuongezeka kwa wataalamu wengi watakaoendelea kutekeleza shughuli mbalimball, kuongeza ajira , kuimarisha usafiri na Itasaidia kuondoa vikwazo vya biashara, kuchochea shughuli zingine za utalii.
''Maelekezo ya Rais ni kuona maziwa haya yanakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi na ndio kitu ambacho kimetufikisha hapa na ndio maana kuna jambo pekee Katika miaka hii mitatu ukichukua mikataba iliyofanyika katika kipindi hiki haijawai kutokea uwekezaji mkubwa uliofanyika kama huu,"Erick Hamis,Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya huduma za Meli.
Pia ameendelea kubainisha leo tumeona utiaji saini wa mikataba mitatu ya ukarabati wa Meli, watu wa kigoma leo watakuwa na furaha kusikia habari hii,tukio la leo linadhihirisha dhamira ya dhati na kivitendo tumshukuru Rais Samia kwa dhamira yake ya kuboresha meli hizo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.