Serikali imesema haitarajii kuona ndani ya miaka 10 kunatokea tena uchakavu wa rejareja wa majengo ya shule 17 kongwe nchini ambayo yamefanyiwa ukarabati mkubwa uliogharamu kiasi cha Sh bilioni 19.2 ambazo ni kodi ya watanzania.
Hivyo imewataka wakuu wa shule, bodi na kamati za shule kuhakikisha zinawajibika kutunza na kusimamia rasilimali hizo kikamilifu na inapotokea uharibifu wa aina yoyote ile ukiwamo kioo kunyofoka hatua zichukuliwe haraka ili kuepuka hasara kubwa.
Kauli hiyo imetolewa Mkoani Mwanza na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako wakati akikiagua na kupokea majengo ya shule ya sekondari ya Bwiru wasichana na Sengerema wavulana yaliyofanyiwa ukarabati chini ya usimamizi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).
Profesa Ndalichako alisema Serikali imetumia kiasi kikubwa kukarabati na kujenga baadhi ya majengo mapya katika shule kongwe 17 nchini, hivyo ni wajibu wa watumishi wa umma kuyatunza ili yaweze kutumika kuzalisha taaluma bora kwa wanafunzi.
“Serikali iliamua kuboresha majengo ya shule kongwe hapa nchini, nakumbuka mwaka 2016 tulianza na shule 10 kwa kutumia wakandarasi lakini baadaye tulibaini kuna gharama na kazi inachelewa kukamilika, katika awamu ya pili tuliamua kubadilisha mfumo na kuja na ujenzi shirikishi kwa jamii ambapo tulitumia wataalamu wetu wa vyuo vya sayansi kutushauri na tumefanikiwa.
“Awamu hiyo ya pili tulitenga fedha tena kwa shule saba zikiwamo ya Sengerema Wavulana na Bwiru za hapa Mwanza, hakika kazi imefanyika nzuri sana ambayo hatukututegemea kwani baadhi ya fedha zilibaki na zikatumika kujenga majengo mengine mapya, pongezi hizi ziende kwa TEA ambayo ilipewa kazi kusimamia sughuli hii, wameonyesha uzalendo na utendaji uliotukaka.
“Rais wetu Mhe. Dkt. John Magufuli anataka kodi ya watanzania ifanye vitu vinavyoonekana kwa macho ya watu wote, ndiyo maana mnashuhuhudia miradi inaibuliwa ambayo kila mmoja anaiona na inatekelezwa kwa faida ya watu wote, wito wetu kwa wakuu wa shule na kamati na bodi zote, hatutaki kuona uchakavu wa rejareja eti kioo kimenyofoka mnakaa kimya bila hatua, hatutarajii ndani ya miaka 10 jengo limechakaa kila mmoja awajibike kuyatunza na yatumike kuinua taaluma kwa wanafunzi,”alisema.
Profesa Ndalichako alisema si kwamba shule kongwe zipo 17 nchini zilizochakaa, la hasha bali wameanza na hizo na wataendelea na zingine 82 kadri fedha zitakavyopatikana ikiwa lengo ni kutaka kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu ili watanzania wapate taaluma yenye viwango na watumishi wafanye kazi mazingira yanayovutia.
Vile Vile alisema Serikali imeanza kukarabati na kujenga majengo mapya katika vyuo vikuu vyote nchini ikiwa lengo ni lile lile la kuboresha miundombinu ya sekta ya elimu ambapo aliahidi kwamba miaka miachache ijayo kilio cha nyumba za walimu kitaisha kwani wamejipanga kuondoa changamoto hiyo.
Akikabidhi majengo hayo kwa Profesa Ndalichako, Mkurugenzi Mtendaji wa TEA, Bahati Geuze, aliishukuru Serikali kwa kuwaamini kusimamia ukarabati wa shule kongwe nchini na shughuli hiyo wameifanya kwa uadilifu mkubwa sana.
Alisema gharama zilizotumika kukarabati na kujenga baadhi ya majengo mapya katika shule kongwe 17 chini ni Sh bilioni 19.28 ambapo kwa upande wa sekondari ya wasichana zilitumika Sh. milioni 974 huku Sengerena wavulana zilitumika Sh bilioni 1.2.
“TEA inaahidi kuendelea kukarabati shule zilizochakaa na kufuatilia kwa ukaribu miradi ya shule, moja ya changamoto iliyokuwa ikitukabili wakati wa utekelezaji ni baadhi ya shule gharama kuongezeka kwani unaponza kuboresha eneo moja, tatizo linguine linajitokeza tena hivyo lazima litatutuliwe ili ujenzi uendelee,”alisema.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.