Waandishi wa Habari kutoka mikoa saba ya Kanda ya Ziwa, wamepatiwa mafunzo ya namna wanavyoweza kutumia mbinu mbalimbali kuhakikisha usalama wao wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.
Akitoa taarifa wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa (UNESCO) Tanzania Dr. Moshi Kimizi alisema, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo waandishi wa habari husasani wa vijijini kuhusu njia bora za kufanya kazi zao kwa ufanisi, usalama na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini .
"Katika nchi mbalimbali duniani waandishi wanafanya kazi katika mazingira magumu na hatarishi, takwimu zinaonyesha kwamba, duniani mwandishi mmoja anauwawa kila baada ya siku tano katika harakati za kutekeleza majukumu yake ya kiuandishi ambapo katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara waandishi 73 walipoteza maisha kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita,"alisema Kimizi.
Aliongeza kuwa, katika baadhi ya nchi duniani, mamia ya waandishi wa habari wanauawa, wanatekwa, wanatishwa, wananyamazishwa, wanadhalilishwa na kuwekwa chini ya ulinzi bila kufuata sheria kwa sababu ya kusema ukweli kwa kueleza maovu mbalimbali yanayoidhuru jamii husika, ndiyo chachu iliyowafanya UNESCO kuandaa mafunzo hayo.
"Mtajifunza na kujadili mada mbalimbali zinazolenga kuimarisha uandishi wenu katika mtazamo wa usalama ambapo, baadhi ya mada nyeti zikiwa ni kujifunza sheria za uandishi wa habari, maadili ya uandishi wa habari, sheria za habari za kimataifa ambazo Tanzania inazitambua, sera za vyombo vya habari, bima kwa waandishi wa habari na namna nyingine za kuhakikisha usalama wao pamoja na mikataba ya ajira, hivyo baada ya mafunzo hayo kila mmoja atayatafasiri kwa vitendo ili kuepukana na habari zinazoweza kuwaletea madhara," aliongeza.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Mhandisi Warioba Sanya ambaye alizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongella alisema, suala la usalama na ulinzi kwa waandishi ni lenye umuhimu hasa ukizingatia majukumu mahasusi waliyonayo ya kuahabarisha ,kuuelimisha na kuushawishi umma kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo na ustawi wa jamii.
Alisema, pamoja na umuhimu huo wa waandishi, takwimu na taarifa za mashirika mbalimbali husasani UNESCO zinaonyesha kuwa takriban waandishi 820 wanauawa katika kipindi cha miaka 10 iliyopita wakati wakitimiza majukumu yao ,ili kufahamu njia bora zinazopatikana kwa urahisi Serikali kwa kushirikiana na tume hiyo imechukua uamuzi mahsusi wa kufanya uwezeshaji na kuendesha mafunzo hayo.
" Nimetaarifiwa mafunzo hayo yatafanyika hapa Mwanza na huko Dodoma yakishirikisha waandishi kutoka takriban mikoa yote ya Tanzania ambapo kwa hapa wametoka Mwanza, Shinyanga, Tabora, Geita, Mara, kagera na Simiyu hivyo matumaini yangu kwa kupitia mafunzo haya tunaweza kuona mabadiliko makubwa katika sekta ya uandishi wa habari husasani usalama na ulinzi wakiwa kazini," alisema Sanya.
Kwa upande wake mmoja wa wakufumzi wa mafunzo hayo kutoka chuo kikuu cha Dar es salaam kupitia shule kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) Dotto Kuhenga alisema, mara nyingi waandishi wa habari wanasahau ulinzi na usalama wao wakati wa majukumu yao hivyo ni wakati kutambua na kuzielewa njia za kujilinda dhidi ya hatari yoyote inapojitokeza ili kupunguza ongezeko la waandishi kupoteza maisha.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.