Mkuu wa Wilaya ya Sengerema Mhe.Emmanuel Kipole kwa niaba ya Mkuu wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe.John Mongella ametoa vitambulisho 23 kwa wakaguzi wa Mazingira kutoka Mamlaka za Serikali za Mitaa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Vitambulisho hivyo vimetolewa kufuatia kifungu cha 183(2) cha Sheria ya usimamizi wa Mazingira,Baraza la Usimamizi wa Mazingira Makao Makuu lilitengeneza vitambulisho 23 kwa ajili ya maafisa walioshiriki mafunzo ya wakaguzi wa Mazingira, ambapo walengwa wamekabidhiwa vitambulisho hivyo ili waweze kushiriki kwa ukamilifu kwenye usimamizi na ufuatiliaji wa katazo la matumizi ya mifuko ya Plastiki.
"Zoezi hili ni la kishwria kama Mkoa hatutaki kusikia linafanyika tofauti na Mikoa mingine maana maelekezo ni yaleyale na yametolewa na mtu mmoja ambaye ni Makamu wa Rais kila mmoja afuate sheria.
"Anayestahili kupigwa faini apigwe kiharali bila kuaangalia chwo wala kiwango cha fedha alizonazo, kazi hii isiwe ya rushwa naombeni mkafanye kazi kwa uwazi, " alisema Mhe Kipole.
Pamoja na kukabidhiwa vitambulisho hivyo,moja ya mamlaka waliyopewa ni kuingia kwenye jengo lolote,ndani ya ndege, chombo cha majini,ardhini au sehemu yoyote isiyo na makazi ya watu.
Pia kusimamisha chombo chochote na kufanya ukaguzi,kuchukua sampuli,kupiga picha,kukamata chombo na kutoa agizo kwa mujibu wa sheria.
Akiongea katika makabidhiano hayo Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Christopher Kadio amesema tarehe 12 hadi 14 desemba 2018 Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira lilifanya mafunzo kwa wakaguzi 23 wa Mkoa wa Mwanza.
"Lengo ilikuwa ni kuwajengea uwezo wa kufanya ukaguzi wa mazingira pamoja na kuwakumbusha maadili wakati wa utekelezaji wa majukumu ya Wakaguzi wa Mazingira kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Na.20 ya Mwaka 2004, alisema Kadio".
Aidha, Kadio ameongeza kuwa wateuliwa wamekidhi sifa za kuwa Wakaguzi wa Mazingira zilizoelekezwa na Ofisi ya Makamu wa Rais ambazo ni uadilifu wa Mtumishi na asiwe na taarifa za Uhalifu, awe na uchapakazi na ushirikiano, awe mtumishi yeyote wa Umma na awe na Taaluma yoyote inayohusiana na Shughuli za Mazingira.
Hata hivyo Mmoja kati ya wakaguzi waliopata vitambulisho hivyo kutoka Wilaya ya Magu Ngusa Buyamba amesema dhamana waliyopewa ni kubwa hivyo wataitendea haki ili kuepuka kutokuelewana kwa Serikali na wananchi.
"Ahadi yetu ni uadilifu majukumu tuliyopewa ni makubwa naombeni uamuzi wa mwisho uhusishe mwajili wako," alisema Buyamba.
Kwa upande wake Afisa Misitu na Mratibu wa Shughuli za Mazingira Mkoa wa Mwanza Mangabe Mnilago amesema Serikali imewaamini na kuwapa mafunzo hivyo watahakikisha wanatenda haki na kutimiza wajibu wao ili mazingira yawe salama kila mmoja atimize azma ya Serikali ya kutunza mazingira.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.