Wamiliki wa Vyombo vya usafiri wa majini wametakiwa kuzingitia uwezo wa vyombo vyao badala ya kuendekeza tabia ya kuhesabu abiria wanaoingia kwenye chombo na kuhatarisha usalama wao na chombo.
Rai hiyo imetolewa jijini Mwanza na Meneja Usajili, Ukaguzi na Udhibiti wa Vyombo vya Majini wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Mhandisi Alfred Waryana, baada ya kutembelea kivuko cha Kamanga Ferry.
Alisema wamiliki wa vyombo vya usafiri wa majini pamoja na wafanyakazi wao, wazingatie utaratibu wa kupakia abiria na mizigo ili kulinda usalama wa watumia huduma na kuepusha madhara na ajali za majini.
Mhandisi Waryana ambaye ameongozana na wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa TASAC na Menejimenti ya shirika hilo, amewaagiza manahodha kuwaelimisha abiria kuhusu matumizi ya vifaa vya kuokolea maisha kabla ya chombo kuondoka gatini na kuwataka wamiliki kuajiri manahodha na mabahari wenye viwango vinavyotambulika.
“Nitoe rai kwa wamiliki na wafanyakazi kuacha tabia ya kuhesabu abiria wanapoingia kwenye chombo badala ya kuzingatia uwezo wa chombo ili kulinda usalama.Pia wazingatie utaratibu wa kupakia na kupanga aina ya mizigo na ipangwe kabla ya abiria kuingia ndani ya chombo,”alisema Mhandisi Waryana.
Alieleza kuwa manahodha wa vyombo wahakikishe wanasimamia upangaji wa mizigo yote kwenye vyombo na kuonya kuwa watafanya makosa endapo wataacha jukumu hilo kusimamiwa na watu wasio na utaalamu jambo linaloweza kusababisha ajali kutokana na upangaji mbaya wa mizigo.
Aidha,alisistiza kuwa chombo kinapofika ng’ambo ya pili sharti abiria washuke kwanza kabla ya magari ili kuzuia mwingiliano na kwamba vyombo vya majini kabla ya kuanza kutoa huduma vinatakiwa kukaguliwa,kusajiliwa na kupewa vyeti na hivyo wamiliki wazingatie masuala hayo kwa kuwa ni ya msingi.
Meneja udhibiti na usajili huyo aliongeza kuwa ukaguzi unaofanyika huainisha vifaa vyote vinavyotakiwa kwenye chombo, sifa za manahodha na mabaharia na mfumo wa upakiaji abiria na mizigo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.