WAZIRI MKUU AONGOZA KONGAMANO LA MAFIGA MATATU LA UONGOZI WA RAIS SAMIA MWANZA
*Majaliwa apongeza Mkoa na wanahabari Mwanza kwa kongamano lenye tija*
*Asema ujenzi wa Meli na Bandari ukanda wa ziwa Victoria kuimarisha usafirishaji*
*Mkuu wa Mkoa asema shule mpya 11 zajengwa ndani ya miaka mitatu*
*Wadau wasifia upatikanaji wa pembejeo za kilimo na kuimarika kwa bei za mazao*
*Siasa za kistaarabu na uhuru wa kuongea ni alama ya demokrasia kuimarika*
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa (MB) leo Machi 30, 2024 ameongoza Mdahalo wa wazi ulioandaliwa na wanahabari Mkoani Mwanza ulioangazia mafanikio ya miaka mitatu ya uongozi wa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Majaliwa ametumia wasaa huo kupongeza Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na wanahabari kwa kongamano hilo lenye jina la 'Mafiga Matatu' ili kuelimisha na akatoa rai kwa vyombo vya habari kuhamasisha umma kushiriki katika mchakato wa kuleta maendeleo nchini ambayo Rais Samia amekua kiongozi.
Waziri mkuu amesema Serikali ya awamu ya sita imeendelea kuimarisha ulinzi na usalama nchini pamoja na uchumi ambapo sasa Mataifa ya nje yamekua yakivutiwa na diplomasia ya nchi huku akitaja ufunguzi wa balozi mpya kwenye mataifa mbalimbali kama ishara ya kuzidi kukubalika.
Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhe. Hassan Masala ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilemela amesema katika Sekta ya Elimu katika kipindi cha miaka 3 zimejengwa shule mpya 11 na vyumba vya madarasa 989, mabweni ya wanafunzi 30, nyumba za walimu 12, matundu ya vyoo 133 katika Shule za Sekondari.
"Shule za Msingi zimeongezeka kutoka shule 958 mwaka 2020 hadi 1,043 kwa sasa, hili ni ongezeko la shule 85 za msingi sawa na asilimia 8.1 na
kwa upande wa shule za Sekondari mwaka 2020 kulikuwa na sekondari 275, kwa sasa ziko shule 332 ikiwa ni ongezeko la shule 57 sawa na asilimia 17.1 na shule za sekondari zenye madarasa ya kidato cha 5 na 6 zimefikia 39, kutoka shule 31 mwaka 2020." DC Masala.
Prof Issa Musoke ametumia jukwaa hilo kupongeza Serikali kwa uboreshaji wa huduma za jamii hususani Sekta ya Elimu ambapo amesifu kwenye kutoa Elimu bila malipo hadi kidato cha sita pamoja na upanuzi wa wigo kwenye Mikopo ya Elimu ya juu huku akibainisha kuwa mtoto wa kike amewekewa mazingira sawa na wa kiume.
Akizungumzia suala la ujenzi wa miradi mikubwa nchini, Mhadhiri Mwandamizi wa Uchumi kutoka SAUT Dkt. Anagongwe Ngowi amesema inasaidia wananchi kupata ajira kwenye miradi hiyo na Serikali inapofanya matumizi kwenye ununuzi wa vifaa na huduma kutoka nchi kadhaa inakuza uchumi wa nchi.
"Mwanzo watanzania wengi hawakuamini kwamba Rais Samia angeweza kuendeleza na kuanzisha miradi ya kimkakati nchini lakini sasa wanaona jinsi uchumi wetu unavyoimarika kutokana na msimamo na mtazamo wake unaomuweka kwenye ramani ya ubora," amesema Mzee Hamduni Marcel wakati akichangia mada.
Mratibu wa Mdaharo huo Aloyce Nyanda amesifu uvumilivu wa Serikali ya awamu ya sita kwa kuwa tayari wakati wote kusikia ukosoaji wa wadau kwenye maeneo mbalimbali yanapoonesha kwenda vibaya kwa ajili ya kujirekebisha huku akimtolea mfano Waziri Mkuu aliyeitikia wito kwenye mdaharo huo.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.