Bodi ya Barabara Mkoa wa Mwanza imetakiwa kusimamia kwa ufanisi utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara kwa kuhakikisha inazingatia ubora unaoendana na thamani ya fedha zinazotolewa na Serikali.

Rai hiyo imetolewa leo tarehe 08 Januari 2026 na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Christopher Ngubiyagai alipokuwa akifungua Kikao cha Kwanza cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mwanza kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Mhe. Ngubiyagai amesema ili kufikia malengo ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika sekta ya miundombinu, hususan kuhakikisha barabara zote nchini zinapitika katika vipindi vyote vya mwaka, ni lazima watendaji kubadili fikra, kuongeza uwajibikaji na kufanya kazi kwa kujituma zaidi.

Amesisitiza kuwa vikao vya bodi vinapaswa kuwa chachu ya kutatua changamoto zilizopo badala ya kuwa majukwaa ya majadiliano pekee, akihimiza utekelezaji wa maamuzi yanayofikiwa.

“Kupitia vikao vya bodi tuhakikishe tunapokea na kujadili changamoto zilizopo, na baada ya kikao kila mmoja akasimamie utekelezaji wa maazimio ili wananchi wanufaike kwa kusafirisha mazao yao na kutumia barabara kwa usalama”. Amesema Mhe. Ngubiyagai.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Buchosa Mhe. Eric Shigongo ameihoji bodi hiyo juu ya kuchelewa kuanza kwa ujenzi wa barabara ya Sengerema–Nyehunge licha ya mkandarasi aliyeshinda zabuni hiyo kusaini mkataba.

“Mkandarasi tayari amesaini mkataba wa ujenzi wa barabara hiyo lakini bado hajaanza kazi. Ni lini ataanza ujenzi maana wananchi wanateseka kutokana na mashimo mengi yaliyopo kwenye barabara hiyo”. Amehoji Mhe. Shigongo.

Akijibu hoja hiyo, Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mwanza Mhandisi Pascal Ambrose amesema Serikali inatarajia kumlipa mkandarasi huyo malipo ya awali, hatua itakayomwezesha kuanza utekelezaji wa mradi huo hivi karibuni.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo ni miongoni mwa miradi muhimu itakayosaidia kuboresha usafiri, kuchochea shughuli za kiuchumi na kupunguza kero kwa wananchi wa maeneo yanayohudumiwa na barabara hiyo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.