DARAJA LA KIGONGO-BUSISI KUANZA KUTUMIKA MUDA WOWOTE KUANZIA SASA.
Serikali imetangaza kuwa daraja la JPM Kigongo-Busisi, linalounganisha wilaya za Sengerema na Misungwi mkoani Mwanza lipo tayari kuanza kutumika muda wowote kuanzia sasa baada ya kukamilika kwa zaidi ya asilimia 99 ya ujenzi wake.
Taarifa hiyo imetolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa wakati wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya kimkakati mkoani Mwanza ikiwemo ya vivuko na daraja hilo muhimu.
Msigwa amesema kukamilika kwa daraja hilo ni hatua kubwa ya maendeleo kwani linakwenda kumaliza changamoto ya usafiri kwa wananchi wa mikoa ya Kanda ya ziwa na hata wale wanaotoka nje ya nchi wanaovuka ziwa Victoria kuingia au kutoka mkoani Mwanza.
“Daraja hili linatarajiwa kuanza kutumika ndani ya mwezi Mei.Hii ni neema kwa Watanzania, hususan wa mikoa ya kanda hii, kwani litaimarisha biashara, usafiri na fursa nyingine za kiuchumi,” amesema Msigwa.
Aidha, Msigwa amesema serikali inaendelea kutekeleza miradi mingine ya kuboresha usafiri wa majini kwa kujenga vivuko vipya katika maeneo mbalimbali ya Ziwa Victoria ili kurahisisha huduma kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Msigwa ametembelea pia ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza ambao umefikia asilimia 96. Alisema kazi zilizobaki ni kufunga viti na vitanda, na meli hiyo itaanza kutoa huduma kwa wananchi muda si mrefu.
Ameeleza kuwa miradi hii yote ni sehemu ya dhamira ya serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha miundombinu ya usafiri na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na Taifa kwa ujumla.
Katika ziara hiyo, Msigwa aliambatana na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Mwanza na Shinyanga, waliopata fursa ya kujionea maendeleo ya utekelezaji wa miradi hiyo ya kimkakati.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.