Mkuu wa Wilaya ya Ilemela Mhe. Amir Mkalipa amevipongeza vikundi vya mbio za pole pole (Jogging) mkoani humo kwa kuandaa tamasha la kuwahamasisha wananchi kufanya mazoezi kwa ajili ya kulinda afya zao dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.

Amesema hayo akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa Mwanza katikaTamasha la mbio za pole zenye lengo la kujenga afya na kupongeza maboresho katika sekta ya afya lililofanyika leo Oktoba 25, 2025 kwa kukimbia kuanzia viwanja vya Furahisha hadi hospitali ya Rufaa ya Mkoa Sekou-Toure, kuchangia damu pamoja na kufanya usafi katika hospitali hiyo.

Ameongeza kwa kuishukuru serikali ya awamu ya Sita kwa kuboresha sekta afya mkoani humo kwa kuongeza ajira na kupunguza uhaba wa watumishi, kuleta vifaa tiba, madawa pamoja na kuboresha huduma za kibingwa katika hospitali ya Mkoa ya rufaa Sekou-Toure na hospitali ya kanda Bugando.

“Zaidi ya watumishi 600 wameongezeka sekta ya Afya mkoani Mwanza huku huduma za matibabu ya saratani zikipatikana katika hospital ya kanda Bugando na dawa zikipatikana kutoka asilimia 75 na kufikia asilimia 97 kwa kipindi cha miaka minne iliyopita”. Amesema Mhe. Mkalipa.
Sambamba na hayo Mhe. Mkalipa amewataka wananchi Mkoani Mwanza kuendelea kuilinda amani ya Mkoa na nchi kwa ujumla huku wakijitokeza kushiriki katika zoezi la kupiga kura kwa amani na kuchagua viongozi ambao wataleta maendeleo yenye tija katika taifa na maeneo yao wanayoishi.

Naye Msimamizi wa kituo cha michezo Biro na muandaaji wa tamasha la mbio za pole Bw. Hamisi Bilali amesema lengo kuu la kuandaa tamasha hilo ni kupongeza maendeleo yaliyofanyika ndani ya serikali ya awamu ya Sita katika huduma za afya na kuwahimiza wananchi kutunza afya zao.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba amesema sekta ya afya imeendelea kua bora kwa kutoa huduma za matibabu ya dharura katika hospitali za Halmashauri zote, uboreshaji wa mashine za Xray, CT Scan na utra sound sambamba na hayo serikali imetoa fedha Bilioni 25 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya rufaa katika wilaya ya Ukerewe.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.