Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kuhakikisha wanachangamkia fursa ya uwepo wa 30% ya Makundi maalum ili yaweze kunufaika.
Dkt. Jingu ameyasema hayo leo julai 03, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mwanza kuhusu ushiriki wa Makundi maalum katika 30% ya zabuni za umma, na kuwataka kuhakikisha wale watu wote wanaohitaji usaidizi na wenye sifa wanaunganishwa na wadau wanaohusika ikiwemo vitengo vya manunuzi.
“Sisi kaka watendaji jukumu letu kwenye maeneo yetu ni kuhakikisha makundi haya yanakuwepo na yanashughulikia tenda hizi”. Amesema.
Kadhalika, Katibu Mkuu huyo amesema sera ya serikali ni kuwa na uchumi na maendeleo jumuishi na asiwepo mtu wa kubaki nyuma na wote wakiwezeshwa watakuwa wamepambana na umaskini, utegemezi na unyonge.
“Yote haya tukiyafanya tutakuwa tunaiendeleza jamii na tutakuwa tunatimiza adhma yetu”. Ameongeza Dkt. Jingu.
Aidha, Dkt. Jingu amewataka Maafisa maendeleo ya jamii kutoka kila Halmashauri nchini kujitahidi walau kuwa na vikundi visivyoupungua 20 ambavyo vitakua vimesajiliwa kwenye mfumo wa manunuzi na viwe na sifa kushiriki katika mchakato wa manunuzi.
Sambamba na hayo, ameagiza zichukuliwe hatua za makusudi za kuviunganisha vikundi hivyo na fursa zilizopo, fursa za manunuzi kwenye Taasisi mbalimbali za serikali na fursa kwenye maeneo mengine ikiwemo sekta binafsi.
Naye Mkurugenzi Msaidizi idara ya Maendeleo ya jinsia Bi. Juliana Kibonde amesema lengo la mafunzo hayo ni kuhamasisha na kusisitiza umuhimu wa urasimishaji wa makundi maalum na umuhimu wa kufikisha elimu hiyo kwa jamii pamoja na kujenga uelewa katika ushiriki wa makundi maalumu juu ya ununuzi wa umma.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.