Katibu Tawala wa Mkoa wa Mwanza Bw. Balandya Elikana amezitaka Halmashauri za Mkoa wa Mwanza kuwachukulia hatua wazazi na walezi ambao wanakiuka sheria na kanuni za malezi ya watoto ikiwemo kuruhusu watoto kwenda mtaani.
Bwana Balandya ametoa rai hiyo leo tarehe 10 Septemba, 2025 wakati akihutubia katika hafla fupi ya kuwatunukia vyeti wahitimu 165 kutoka kwenye vituo vya kulea watoto ambao wamepata mafunzo ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto ikiwa ni katika harakati za kumlinda mtoto na ukatili.
Akijibu risala ya washiriki wa mafunzo Bw. Balandya amewataka Maafisa maendeleo ya jamii kuwasaidia wananchi kuzitambua fursa za kuinua kipato na uchumi zilizopo katka jamii na kuwajengea uwezo ili wajiunge kwenye makundi na kuweza kupata mikopo isiyo na riba.
"Maafisa maendeleo ya jamii mnatakiwa kuwasaidia wananchi kuhakikisha wanatambua na kuzielewa fursa zilizopo katika jamii zetu ambazo zinaweza kuinua kipato chao kwa mfano fursa za mikopo inayotolewa kwa ajili ya kufanya uvuvi wa kisasa wa vizimba." Amesema Bw. Balandya.
Naye, Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt. Jesca Lebba amewashukuru wadau waliofadhili mafunzo hayo (RCA) pamoja na wakufunzi na wanafunzi walioungana kwa pamoja kuhakikisha wanapata stadi za kuwalinda watoto na jamii na kwamba wahakikishe wanafikisha elimu hiyo kwa kundi kubwa zaidi la wazazi na walezi ambao hawakupata.
Kwa upande wake mwakilishi kutoka shirika lisilo la kiserikali la Railway Children Afrika (RCA) Bw. Renatus Fuastine wamelenga kuwafikia walezi wa watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0-8 ambao wameramani kuona watoto wanaishi kwenye familia zao na sio kuishi mtaani kwa kuwafikia wazazi kwenyw jamii na kuwapa elimu.
"Tuna matumaini walezi mliopata mafunzo haya mtawafikia wazazi na walezi wengi zaidi ambao hawakupata mafunzo haya ili muweze kuwapa elimu hii ili tuondokane na ukatili wa watoto na wanawake, nyie mmeshakua mabalozi na tunawategemea na kwa siku za usoni tutawafikia wengine nje ya Nyamagana na Ilemela", amesisitiza.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.