Mojawapo ya vitu ambavyo mkoa wa Mwanza unajivunia katika mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani, ni uendelezwaji na uanzishwa wa miradi ya maendeleo.
Taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 katika sekta za elimu, afya na maji inasema mkoa wa Mwanza umepokea Sh.35, 493,712,833.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi hiyo.
Kati ya fedha hizo Sh. 20,500,000,000 ni kwa ajili ya kutekeleza Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa katika sekta ya elimu, Sh. 10,493,712,833.3 kwa ajili ya Mapambano dhidi ya Uviko-19 katika sekta ya afya na Sh.4,500,000,000 kwa ajili ya mapambano dhidi ya Uviko-19 katika sekta ya maji.
Kwa mpango wa maendeleo kwa ustawi wa taifa, Mkoa umepokea kiasi cha Sh. 20,500,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 1,017 na mabweni mawili. Kati ya fedha hizo, Sh. 19,700,000,000 ni kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 985 kwa shule za sekondari, Sh. 640,000,000 vyumba vya madarasa 32 vya vituo shikizi shule za msingi katika Halmashauri za Wilaya za Buchosa, Sengerema na Ukerewe na Sh. 160,000,000 ujenzi wa mabweni ya shule za msingi zenye wanafunzi walio na mahitaji maalum katika Halmashauri za Wilaya za Ukerewe na Sengerema.
Kwa mapambano dhidi ya uviko – 19, Mwanza imepokea Sh. 10,493,712,833.3 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya afya.
Mkuu wa Mkoa (RC), Robert Gabriel anamshukuru Rais Samia kwa kutoa fedha ya kutekeleza miradi hiyo, na wananchi pia wanaeleza matumaini yao kwa serikali ya awamu ya sita juu ya uboreshaji endelevu wa huduma muhimu za kijamii.
SEKTA YA AFYA
Miongini mwa wananchi wanaoeleza imani yao kwa Rais Samia ni wakazi wa Kata ya Buhongwa wilayani Nyamagana ambao walishindwa kuzuia furaha zao mwezi uliopita, baada ya Mkuu wa Mkoa kuwakabidhi kituo cha Afya cha Bulale.
Bulale iliku ni zahanati, ikafanyiwa ukarabati na kupandishwa hadhi kuwa Kituo cha afya kinachowanufaisha wakazi 16,113.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Dk Sebastiani Pima anasema jiji lilipokea Sh milioni 250 mwezi Agosti, 2021 kwa ajili ya upanuazi wa kituo hicho, uliohusisha ujenzi wa wodi ya wazazi, maabara, mashimo ya maji taka na kichomea taka.
“Mradi huu una faida nyingi kwa wananchi, ikiwemo kupunguza vifo vya mama wajawzito na watoto wachanga kutokana na huduma za afya kuwa karibu na wananchi,” anasema.
Mkazi wa Mtaa wa Bulale, Ester Kisena, anaishukuru serikali kwa hatua hiyo ambayo imewasogezea huduma karibu kwani awali walikua wakilazimika kusafiri umbali mrefu hadi hospitali ya Wilaya Nyamagana, Butimba.
Anasema wananchi wako tayari kuendelea kuchangia nguvu na ujuzi kwa upanuzi zaidi wa kituo hicho, ikiwemo ujenzi wa jengo la upasuaji, la kuhifadhi maiti na nyumba ya watumishi.
SEKTA YA ELIMU
Kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa Mkoa, Martin Nkwabi, maendeleo ya elimu yanaimarika kwa kasi, hasa uboreshaji wa miundombinu ambapo Halmashauri za Ilemela, Magu, Sengerema, Ukerewe na Mwanza jiji tayari zimekamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa.
“Ujenzi unaendelea katika Halmashauri za Kwimba na Buchosa , ambayo pia sio muda mrefu vyumba hivyo vitakamilika,” anasema.
Mkuu wa Wilaya ya Magu, Sallum Kalli, anaishukuru serikali kupitia Rais Samia kwa kutafuta fedha zilizowezesha kujengwa madarasa ya shule za msingi zaidi ya 3,000, kwa wakati mmoja wilayani mwake.
“Hili halikuwa jambo rahisi, tumshukuru Mungu kwa kumpa maono Rais ya kutafuta fedha. Huko nyuma tulikuwa tunajenga madarasa manne hadi matano kwa mwaka kwa kutumia fedha za halmashauri. Upande wa sekondari nimemaliza ujenzi wa madarasa 123 na nimetengeneza madawati 4, 920,” anasema.
Mkuu wa Mkoa anazungumzia tena jitihada hizo za Rais Samia, kwamba zinaleta mchango mkubwa kwenye sekta za kiuchumi, akawataka viongozi na watendaji wote wa serikali, wakuu wa wilaya na wakurugenzi watendaji kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi yote, kukemea vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, ambavyo vinakiuka maadili ya utumishi wa umma.
“Tunahitaji kila mwananchi kujikomboa kiuchumi kwa namna mbalimbali kupitia miradi hii, lakini pia awe na uhakika wa kupata huduma zote za kijamii,” anasema.
SEKTA YA MAJI
Katika sekta ya maji, serikali ya awamu ya sita inatekeleza miradi mbalimbali ya maji kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), ikiwemo mitano katika wilaya za Nyamagana na Ilemela, maarufu kama ‘programu na mpango wa maendeleo kwa ustawi wa jamii na mapambano dhidi ya Uviko-19’,
Serikali ya awamu ya sita imetenga Sh. Sh.billion moja kwa miradi hiyo ambayo utekelezaji wake ulianza mwezi Novemba mwaka jana na itaisha mwezi Juni mwaka huu, ingawaje Mkurugenzi wa Mwauwasa, Leonard Msenyele anasema upo uwezekano wa kuisha mwezi ujao, kwani mahitaji yote yapo.
Miradi hiyo ni Bulale, Kambarage, Luchelele, Mlima wa rada na Nyamhongoro, ambayo kwa kiasi kikubwa imewalenga wakazi wa maeneo ya milimani.
Ni kwa sababu hawakuwa wakifikiwa na huduma kutokana na miundombinu iliyopo kutokua na uwezo wa kusukuma maji hadi maeneno hayo.
Msenyele anasema tayari Mamlaka imepokea zaidi ya Sh.400 millioni na utekelezaji umefikia asilimia 40, akasisitiza kwamba: “Tuna imani kabisa hadi mwezi ujao mwishoni wananchi watakua wameanza kupata huduma ya maji safi na salama kwa sababu serikali inatoa pesa kwa wakati kila tunapoomba.”
Anafafanua kwamba zipo sababu nyingi za miradi hiyo kuitwa‘programu na mpango wa maendeleo kwa ustawi wa jamii na mapambano dhidi ya Uviko-19’ kwani upatikanaji wa maji safi na salama kwa ajili ya kusafisha mikono ni mojawapo ya hatua kubwa na muhimu katika kupambana na ugonjwa huo.
Anasema wakandarasi wote wanalipwa kwa wakati na kuongeza kwamba: “Matokeo yake sasa ni kwamba Mamlaka ndioinawadai kazi wakandarasi, wao hawadai hata senti moja. Kwa ujumla tunampongeza Rais Samian kwa ubunifu wake wa kumtua mama ndoo kichwani na sisi wasaidizi wake hatutamuangusha kwani tunafahamu umuhimu wa rasilimali maji katika jamii yetu,” anasistiza.
Kwa mujibu wa Msenyele, ‘programu na mpango wa maendeleo kwa ustawi wa jamii na mapambano dhidi ya Uviko-19’ ni mojawapo miradi iliyoanzishwa na Rais Samia katika sekta ya maji jijini Mwanza.
Wakati huohuo anampongeza Rais kwa kuendeleza miradi iliyoachwa na mtangulizi wake, hayati Rais John Pombe Magufuli (JPM), kwa kutoa pesa kwa wakati, akawataka wananchi kupuuza uzushi wa kwamba miradi ya zamani imesimama.
Anaihakikishia jamii kwamba miradi hiyo ya zamani pia itakamilika kwa wakati, ukiwemo ule wa Butimba, akasema: “Tunaenda na kasi ya mama yetu Samia katika kuhakikisha miradi yote inakamilika kwa wakati ili kuondoa kabisa changamoto za uhaba wa maji.”
MIUNDOMBINU YA BARABARA
Miundombinu ya barabara ni sehemu pia ya miradi iliyopo hatua nzuri za utekelezaji, ikiwemo mradi wa ujenzi wa daraja la Kigongo-Busis, maarufu ‘daraja la JPM’, ulioanzishwa na Rais wa awamu ya tano, hayati Rais Pombe Magufuli (JPM) mnamo mwezi Februari 2020 na unatarajia kukamilika Februari 2024.
Unagharimu zaidi ya Sh.billioni 716 na sasa utekelezaji umefikia asilimia 41.59, ambapo mkandarasi ameshatumia siku 753 kati ya siku 1,461.
Meneja wa wakala wa barabara (Tanroads), Rogatus Mativila, aliiambia kamati ya kudumu ya bunge ya miundombinu kwamba.
“Tunamshukuru Rais Samia kwa kazi nzuri anayoifanya na kazi inaendelea vizuri, tunamaamini utaisha kwa wakati,” anasema.
Mwenyekiti wa Kamati, Seleman Kakoso alimtaka mkandarasi, ambaye ni China Civil Engineering Construction Corporation kuhakikisha anamaliza mradi huo kwa wakati.
“Na vilevile kwenye mradi wowote lazima kuwe na mikataba itakayombana mkandarasi kuhakikisha anaacha fedha za huduma ya kijamii, hilo nalo litekelezwe kama inayotakiwa’’ alisema Kakoso.
Wakati huohuo, Kakoso aliitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kusimamia maslahi ya wafanyakazi wa mradi huo na kuhakikisha yanalipwa kwa wakati.
“Tunapongeza usimamizi. Maendeleo ni mazuri,” alisema.
KAZI IENDELEE.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.