Kikao kazi cha wadau wa Tasnia ya mbegu bora kutoka Kanda ya Ziwa na Magharibi kilicholenga kukusanya maoni ya maboresho ya sheria za mbegu nchini kimefanyika leo mkoani Mwanza.

Kikao hicho, kilichojumuisha wazalishaji, wasambazaji, wataalamu, na wadau wa maendeleo, kililenga kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha sheria na mifumo ya sekta ya mbegu ili kuendana na mahitaji ya kisasa ya kilimo.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Katibu Tawala Msaidizi Sekta ya Uchumi na Uzalishaji, Bi. Kadida Kyamani ametoa wito kwa wadau na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanatumia mbegu bora zilizoidhinishwa, zenye viwango na ubora unaokubalika kitaifa.

Amesisitiza kuwa matumizi ya mbegu bora ni msingi muhimu wa kuongeza uzalishaji wa mazao, kuhakikisha usalama wa chakula na kuinua kipato cha wakulima.

Kadhalika, amehimiza ushirikiano wa karibu kati ya serikali na wadau wa sekta binafsi ili kuendeleza tasnia ya mbegu nchini na kuhakikisha ustawi wa kilimo cha kisasa.

Kikao hicho ni sehemu ya juhudi za kuboresha sekta ya mbegu nchini, kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora zinazofaa kwa mazingira yao na kuongeza tija katika kilimo.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.