MABORESHO YA USAFIRI WA MAJINI USIWAOGOPESHE WAWEKEZAJI-NAIBU WAZIRI
Naibu Waziri wa Uchukukuzi Mhe. David Kihenzile leo amezindua rasmi jina na nembo mpya ya kampuni ya Meli Tanzania, TASHICO na kusisitiza maboresho yanayofanywa na Serikali hayana nia ya ushindani bali ni kurahisisha maendeleo ya wananchi hivyo ni wajibu wote kuunganisha nguvu moja.
Akizungumza katika hafla hiyo leo Novemba 18, 2024 ukumbi wa Kwatunza Hotel wilayani Ilemela Mwanza, Kihenzile amebainisha Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kuiboresha sekta yote ya usafiri ili kujenga uchumi imara kwa maslahi ya wananchi wake na Taifa kwa ujumla.
"Serikali katika miaka hii mitatu imetoa jumla ya Tshs. trilioni 1.2 kwa ajili ya kuboresha miradi ya Meli kwenye maziwa na Mwanza ni Mkoa uliokaa kimkakati kwa kupakana na nchi za Kenya, Rwanda, Burundi na Uganda hivyo mizigo mingi itapita hapa," Naibu Waziri.
Ameongeza kuwa mara reli ya kisasa SGR itakapo kamilika idadi kubwa ya mizigo ya kwenda nchi jirani itaongezeka kutokana na kuimarishwa kwa safari za majini na barabara na hivyo kuzidi kupanua fursa za uwekezaji.
Akitoa salamu za Mkoa wa Mwanza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa,Katibu Tawala wa mkoa huo,Ndugu Balandya Elikana ameishukuru Serikali ya Rais Dkt.Samia kwa kuzidi kuboresha njia kuu za uchumi utakaozidi kuongeza kupata kwa Taifa na maendeleo ya wananchi.
"Hakuna Taifa lolote linaweza kupiga hatua bila ya kuboresha sekta ya uchukuzi,tunaendelea kushuhudia uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali yetu kuanzia upanuzi wa uwanja wa ndege,usafiri wa Meli,barabara na reli ya kisasa.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Meli Tanzania,Meja Jenerali mstaafu John Mbungo ameipongeza kampuni hiyo kwa huduma bora eneo lote la maziwa na kuwataka wazidi kuwa wabunifu katika usafiri huo wa majini.
Awali kampuni hiyo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Kampuni ya huduma za Meli Mwanza MSCL na sasa inajulikana kwa jina la Kampuni ya Meli Tanzania TASHICO
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.