*Makatibu wa Afya nchini watakiwa kupanua wigo wa Ukusanyaji Mapato*
Katibu Tawala Mkoa wa Mwanza Ndugu Balandya Elikana amewataka Makatibu wa Afya Nchini kusimamia Mifumo ya Ukusanyaji Mapato kwenye maeneo yao ya kazi ili kuimarisha taasisi zao kwenye sekta ya Rasilimali fedha.
Balandya amesema hayo leo Mei 19, 2023 jijini Mwanza wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Makatibu wa Afya Tanzania ambao umefanyika Mkoani humo kwenye ukumbi wa Gold Crest kuanzia Mei 16-19, 2023.
"Ni muhimu sana kusimamia vizuri mifumo ili iweze kutuongezea mapato kwani tukijiimarisha kwenye eneo hilo kutasaidia kupata Rasilimali fedha zitakazosaidia kwenye utekelezaji wa majukumu badala ya kusubiri fedha kutoka serikali kuu." Amesisitiza Katibu Tawala.
Vilevile, ametoa rai kwa kundi hilo kwenda kutoa elimu ya mfuko wa fidia kwa wafanyakazi kwa watumishi walio kwenye maeneo yao ili kurahisisha uratibu wa shughuli za mfuko huo na kusaidia watumishi wanapoumia kazini kupata haki zao.
Hata hivyo, amewataka kwenda kusimamia upatikanaji wa takwimu sahihi katika kutoa maamuzi ili maamuzi yoyote yatokane na takwimu sahihi ili kuweka uhalisia wa ushughulikiaji wa masuala mbalimbali.
"Nina imani kuwa ndani ya hizi siku mlizokuwepo hapa mmepeana hamasa na chachu ya kuongeza bidii na kuwezesha utoaji wa huduma bora hivyo twendeni tukaboreshe huduma za takwimu kwenye maeneo yetu." Balandya.
"Nina uhakika maazimio mliyojiwekea ndani ya siku tano za Mkutano huu mtakwenda kuyatekepeza kwa vitendo ili kuongeza ufanisi kwenye huduma" Amesema
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Mwanza Bi Claudia Kaluli wakati akimkaribisha Mgeni Rasmi.
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu wa Afya Bi. Juliana Mawala ametumia wasaa huo kuwaasa Makatibu wa Afya kwenda kujituma kwa dhati ili kuhakikisha wananchi wanahudumiwa ipasavyo na pia ameshukuru Uongozi wa Mkoa kwa ushirikiano.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.