MCHAKATO WA KULIGAWA JIMBO LA MAGU WAANZA RASMI-TUME YA UCHAGUZI
Mwenyekiti wa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele leo Aprili 23,2025 ametangaza rasmi kuanza mchakato wa kuligawa jimbo la Magu kwa kufuata miongozo yote ya kikatiba na ya Tume hiyo.
Akizungumza na wadau wa uchaguzi kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Magu, Mwenyekiti huyo amesema mchakato unaofanywa na Tume yake ni kuja kujiridhisha kutokana na maombi yaliyofanyika kuanzia ngazi ya wilaya hadi Mkoa kabla ya kutangaza rasmi jimbo jipya lililopendekezwa la Sanjo.
"Ndugu wadau mliofika hapa naomba tuelewane vizuri msianze kutoka hapa na kusema tayari Jimbo limegawanywa hapana, tume hii inafanya kazi kwa kufuata miongozo ya katiba ya nchi yetu na vifungu vya tume, tumekuja kujiridhisha kwa kuwasikia kile mlichoamua kwa kufuata vikao halali na sisi pia kupita kulikagua jimbo husika", Mhe.Mwambegele.
Aidha, ameongeza kuwa Tume imetimiza matakwa ya kanuni ya 18 ya kanuni ya Tume hiyo ya mwaka 2024 ya kutembelea majimbo yote likiwemo la Magu yaliyoomba kugawanywa au kubadilishwa majina.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa tume hiyo bwana Greyson Okado akiwaapisha wadau hao kwenye maombi yaliyotumwa amebainisha Jimbo la Magu lina zaidi ya wakazi laki nne, jumla ya kata 25 na endapo ombi lao litakubaliwa Jimbo la Magu litabaki na kata 14 na Jimbo la Sanjo liwe na kata 11 na kila Jimbo litabaki na wakazi zaidi ya laki mbili.
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.