Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Kundo Mathew (Mb) amesema Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maji nchini kwa lengo la kuwaondolea wananchi adha ya ukosefu wa rasilimali hiyo muhimu kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Mhe. Kundo ametoa kauli hiyo mapema leo mkoani Mwanza alipofika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa ajili ya salamu za kikazi, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji inayosimamiwa na Mamlaka za RUWASA, MWAUWASA na SEUWASA katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.

Amesema Wizara ya Maji haiishii tu katika utekelezaji wa miradi mipya, bali pia inafanya mapitio ya vyanzo vya maji ili kubaini uwezo wake, kusimamia matumizi sahihi na kuhakikisha vyanzo hivyo vinalindwa ili viendelee kutoa huduma kwa wananchi kwa muda mrefu.

Aidha, Mhe. Kundo amesema wizara imeweka mikakati madhubuti ya kuzuia upotevu wa maji kwa kukomesha vitendo vya wizi wa maji, uchepushaji na uchakavu wa miundombinu, hatua ambayo inalenga kulinda rasilimali hiyo na kuhakikisha maji yanayozalishwa yanatumika ipasavyo.

Akimkaribisha Naibu Waziri huyo Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Mhe. Christopher Ngubiagai ameipongeza Wizara ya Maji kwa kutekeleza jumla ya miradi mikubwa 75 ya maji vijijini yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 155, pamoja na mradi wa maji wa thamani ya shilingi bilioni 48 unaotekelezwa maeneo ya mjini.

Amesema mradi huo wa mjini ukikamilika utawezesha kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji katika maeneo yenye miinuko, hali ambayo kwa muda mrefu imekuwa kero kwa wakazi wa maeneo hayo.

Halikadhalika, Mhe. Ngubiyagai amewasilisha kilio cha wananchi zaidi ya laki moja wanaonufaika na Mradi wa Maji wa Kiguru–Usagara–Sumve wenye thamani ya shilingi bilioni 41, akiomba utekelezaji wake uharakishwe ili wananchi hao waondokane na adha ya ukosefu wa maji safi na salama.

Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mkoa wa Mwanza, 2 Regional Drive
S.L.P: 119, Mwanza.
Simu: 028-2501037
Simu ya Mkononi: 028-2501037
Barua Pepe: ras@mwanza.go.tz
Hakimiliki©2018. Mkoa wa Mwanza . Haki zote zimehifadhiwa.